
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo
Hussein Bashe ahimiza taasisi za umma na binafsi kuwekeza zaidi katika
uzalishaji mbegu za mazao nchini .Amesema hayo leo jijini Dodoma wakati
wa kikao cha wadau wa mbegu za mazao.
……………..
Serikali imewataka wazalishaji mbegu za mazao nchini kuongeza uzalishaji na ubora ili nchi iepukane na utegemezi toka nje.
Akizungumza katika kikao cha wadau
wa mbegu leo (Jumanne 24.09.2019) jijini Dodoma,Naibu Waziri wa Kilimo
Husein Bashe amesema ili Tanzania ifikie malengo ya kukuza uzalishaji
wenye tija katika kilimo lazima ijitegemee kwa mbegu.
Amebainisha kuwa usalama wa chakula unategemea sana uwezo wa nchi kuzalisha mbegu za mazao ndani na si kutegemea wahisani.
“Kuwa na nchi inayotegemea mbegu
za mazao toka nje kunaondoa dhana ya uhuru na kujitegemea,hivyo
kuhatarisha usalama wa chakula na taifa” alisisitiza Naibu Waziri Bashe
Bashe amewaeleza wadau hao kuwa
Wizara ya Kilimo ina lengo la kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mbegu
hususan zinazozalishwa nchini.
Ameziagiza Taasisi za Utafiti wa
Kilimo(TARI), Kampuni ya Mbegu (ASA) kushirikiana na wadau binafsi
kuwekeza mitaji ili kuinua uzalishaji wa mbegu bora ili kukidhi
mahitaji ya wakulima.
“Ni budi sasa taasisi zetu za TARI
na ASA zikaanza kuzalisha mbegu mara tatu kwa mwaka kwenye mashamba kwa
njia ya umwagiliaji badala ya kutegemea mvua “ Naibu Waziri alisema
Bashe amebainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina utegemezi wa mbegu asilimia 60 kutoka nje ya nchi.
Hali hiyo imesababisha mbegu nyingi kuuzwa kwa bei kubwa na zingine kulalamikiwa na wakulima kuwa na ubora mdogo.
Naibu Waziri Bashe amewataka wadau
kutengeneza mpango maalum wa kuongeza uzalishaji kwani serikali pekee
haiwezi kutokana na soko la mbegu kuwa kubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Mazao ,Wizara ya Kilimo Nyasebwa Chimagu amesema kikao
hicho kitajadili kwa mapana changamoto za upatikanaji mbegu bora na
mfumo mzuri wa usambazaji mbegu nchini.
Nyasebwa aliongeza kusema kwa sasa
wakulima wana malalamiko mengi kuhusu upungufu wa mbegu ,hivyo wizara
na wadau wana jukumu la kutafuta majawabu mapema.
0 comments:
Post a Comment