Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule akitoa nasaha wakati wa kufungua kikao cha utambulisho wa mradi wa Lishe Endelevu unaofadhiliwa na watu wa Marekani (USAID).
Mkuu wa
Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule amepongeza ufadhili wa mfuko wa watu wa
Marekani (USAID) kwa kuujumuisha Mkoa wa Rukwa katika mradi wa Lishe Endelevu,
ili kupunguza na kuondoa hali ya udumavu, Ukondefu, upungufu wa damu kwa watoto
na wanawake pamoja na upungufu wa uzito kwa watoto wachanga katika Mkoa.
Amesema kuwa
kwa muda mrefu mkoa wa Rukwa umeendelea kusikitishwa na takwimu za Utafiti wa
Afya na Idadi ya Watu Tanzania (TDHS) chini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
za mwaka 2015/2016 zinazoonyesha Mkoa wa Rukwa kuwa na kiwango cha asilimia
56.3 ya udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano huku asilimia 5.3 wakiwa
na ukondefu na asilimia 23 wakiwa na uzito mdogo.
Ameongeza
kuwa katika kuhakikisha mkoa unajipanga kukabiliana na hali hiyo hadi sasa Mkoa
tayari umefanikiwa kuandaa mpango mkakati wa lishe wa mkoa wa miaka mitatu
ambao umeanza utekelezaji wake mwaka 2018 na kutegemewa kukamilika mwaka 2021,
amabapo mpango huo umeainisha vipaumbele vya mkoa katika kukabuliana na
utapiamlo ili kuondokana na udumavu.
“Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa amesaini Mkataba wa usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za
lishe na wakuu wa wilaya. Kwa kila robo mwaka taarifa za utekelezaji wa
Mkataba huu hujadiliwa katika Kikao cha mapato na Matumizi cha mkoa. Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa ndio mwenyekiti wa kikao hichi na pia agenda ya lishe imekuwa ni
ya kudumu katika vikao vya kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) pamoja na vikao vya
kamati za ushauri za Wilaya (DCC),” Alisema.
Ameyasema
hayo katika kikao cha utambulisho mradi wa Lishe Endelevu unaofadhiliwa
kwa msaada wa watu wa Marekani unaosimamiwa na shirikia lisilo la Kiserikali la
Save the Children kwa kushirikiana na Delloitee, PANITA, Manoff, na AAPH ambapo
alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliyepaswa kuwa mgeni rasmi katika kikao
hicho kilichowajumuisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wenyeviti
wa halmashauri waganga wakuu wa wilaya na wataalamu kutoka ofisi ya Mkoa na
wawakilishi wa mashirika yanayojihusisha na maendeleo ya afya katika mkoa.
Akielezea
namna ya kushirkiana na uongozi wa Mkoa pamoja na wasimamizi wa mradi
Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi Sichone alilisisitiza
kutomuangusha mkuu wa wilaya katika kutekeleza malengo ya mkoa kuhakikisha
udumavu unapungua ili watoto waweze kulisaidia taifa katika miaka ijayo na
hivyo kuwaasa wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu.
“Ntawataka
wananchi wote katika halmashauri ya wilaya ya Kalambo na maeneo mengine ambapo
mradi huu utapita tuhakikishe tunafuata taratibu ambazo tutaelekezwa na
wataalamu kwamba vyakula hivi ndivyo vinaweza vikatutoa katika hali tuliyonayo
na kwenda katika hali ambayo ni salama
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa mradi huo Bi. Joyceline Kaganda alisema kuwa mradi huo
tayari umeshatambulishwa katika mikoa mingine mitatu ya Dodoma, Iringa na Morogoro
na hivyo kuja kumalizia katika Mkoa wa Rukwa ambapo uzinduzi rasmi wa mradi huo
kitaifa utafanyika Mkoani Rukwa.
“Asilimia
56.3 ya watoto chini ya Miaka mitano wamedumaa hiyo siyo hali nzuri hata
kidogo, hicho ndio kizazi ambacho tunategemea kitakutana na uchumi wa viwanda,
Tanzania inataka kufikia Uchumi wa Kati, tunataka kwenda kwenye uchumi wa
Viwanda, sasa kama hawa watoto wamedumaa, nani atafanya kazi kwenye hivyo
viwanda? Tutafika kwenye lengo? Ndio maana mkoa umechukulia katika hali ya
Uzito,” Alisema.
Malengo ya
mradi huo ni kupunguza udumavu kwa asilimia 15 huku malengo ya mkakati wa lishe
wa Mkoa ni kuhakikisha mkoa unashuka kutoka asilimia 56.3 hadi kufikia asilimia
40 ya udumavu ifikapo mwaka 2021.
0 comments:
Post a Comment