Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga sambamba na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Njombe pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakikagua mabanda mbalimbali wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya chakula Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Mji Mwema mkoani Njombe tarehe 16 Octoba 2020.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akikagua zana mbalimbali za kilimo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya chakula Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Mji Mwema mkoani Njombe tarehe 16 Octoba 2020.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akisisitiza jambo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya chakula Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Mji Mwema mkoani Njombe tarehe 16 Octoba 2020.
Ngoma za asili zikitumbuiza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya chakula Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Mji Mwema mkoani Njombe tarehe 16 Octoba 2020.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akionyesha vitabu mbalimbali vya miongozo nane (8) ya mazao ya bustani vilivyozinduliwa wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya chakula Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Mji Mwema mkoani Njombe tarehe 16 Octoba 2020.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Njombe
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imefanikiwa kuruhusu mazao ya chakula, ikiwa ni pamoja na mahindi kuuzwa nje ya nchi.
Hali hii pia imesaidia kushuka kwa mfumuko wa bei kufikia asilimia 3.86 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 5.59 mwaka 2015. Ili kuboresha masoko kwa mazao ya chakula, hususan mahindi, Serikali imefanikiwa kuanzisha utaratibu wa kutoa vibali mipakani kwa mfumo wa kielektroniki, ambapo waombaji wanapata huduma ya vibali vya kusafirisha nje bila kulazimika kwenda Makao Makuu ya Wizara ya Kilimo.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 16 Octoba 2020 wakati akifunga maadhimisho ya siku ya chakula Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Mji Mwema mkoani Njombe.
Hasunga amesema kuwa Wizara ya Kilimo katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imepata mafanikio makubwa ikiwamo kuchangia nchi kuingia mapema katika uchumi wa kipato cha kati mwaka 2019.
Sekta ya kilimo imefanikiwa kuajili zaidi ya 65% ya nguvukazi na inachangia asilimia 30 ya pato la Taifa (GDP). Aidha, kilimo kinachangia takribani asilimia 65 ya malighafi za viwandani na asilimia 100 ya chakula kinachotumika nchini.
Waziri Hasunga amesema kuwa Chini ya uongozi wa Dkt John Pombe Magufuli yamepatikana mabadiliko makubwa kwenye sekta ya kilimo ikiwemo kuimarika kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo kuiwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula na lishe, upatikanaji wa pembejeo za kilimo na masoko.
Katika Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambayo kaulimbiu yake ni Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora Endelevu, amewataka watanzania kuzingatia kauli mbiu hiyo kwani kwa kushirikiana na wadau, Serikali imedhamiria kutatua changamoto za lishe kwa kuendelea kutekeleza Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe (National Multsectoral Nutrition Action Plan- 2016/2017- 2020/2021) na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP-II).
Ameongeza kuwa Serikali pia kupitia Wizara ya Kilimo na wadau wa lishe nchini imeandaa mwongozo maalum kuhusu vyakula vilivyorutubishwa kibailojia (Biofortification Guidelines) ambao ulizinduliwa kwenye maonesho ya Nanenane tarehe 01/08/2020 na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile katika maadhimisho hayo miongozo mbalimbali yenye kuwaelimisha wataalamu na wananchi kwa jinsi ya kuzalisha, kuhifadhi na kutumia mazao mbalimbali ili kuboresha lishe na kipato katika ngazi ya kaya imezinduliwa.
Aidha, kwa kuwa tupo kwenye kipindi muhimu cha kuamua nchi yetu kupata viongozi bora, napenda kuchukua fursa huii kuwaomba na kuwasihi watanzania kujitokeza kwa wingi ifikapo tarehe 28 Octoba kutumia haki yenu ya kikatiba kuchagua viongozi bora watakaoliongoza Taifa letu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2020-2025.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema kuwa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani 2020 ambayo uadhimishwa kila mwaka, yanafanyika katika kipindi ambacho Dunia inatilia mkazo masuala ya lishe na usalama wa chakula ili kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu ambapo inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 Idadi ya watu itafikia Bilioni 9.
Kusaya amesema kuwa jitihada mbalimbali zinafanywa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuna uwiano sawa kati ya uzalishaji wa chakula na ongezeko la idadi ya watu. Mfano; Azimio la Malabo linatutaka kupunguza upotevu wa mazao ya chakula kwa asilimia 50 ifikapo 2025, malengo endelevu ya millennia yanatutaka kukomesha umaskini na baa la njaa ifikapo 2030 na maazimio mengine ya kikanda na kimataifa hivyo hivyo yanasisitiza kilimo chenye tija kwa ajili ya kumkomboa mkulima hasa wa kawaida.
Katika Maadhimisho hayo Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amezindua Jumla ya miongozo nane (8) ya mazao ya bustani ambapo miongozo saba inahusu kanuni na teknolojia bora za uzalishaji na usimamizi wa mazao ya Bamia, Nyanya, Kabichi, Vitunguu, Mboga za majani, Karoti, Pilipili hoho. Mwongozo wa nane unahusu Kanuni na Tekinolojia bora za Usimamizi wa Mazao ya Mboga na Matunda baada ya kuvuna.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment