METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, March 17, 2019

DKT. NDUGULILE – “WATUMISHI TUISHI KWA UPENDO


 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akisisitiza jambo wakati akiongea na Watumishi wa Sekta ya Afya, katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi kujadili bajeti ya Wizara ya Afya uliofanyika katika ukumbi wa Mipango Jijini Dodoma
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula
Baadhi ya Watumishi wa Sekta ya Afya ambao pia ni Wanachama wa TUGHE Taifa wakishikana mikono huku wakiimba wimbo wa kuhamasisha umoja na mshikamano, wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi kujadili bajeti ya Wizara ya Afya uliofanyika katika ukumbi wa Mipango Jijini Dodoma.

Na WAMJW – Dodoma.

Watumishi watakiwa kudumisha upendo, umoja na mshikamano katika mahala pa kazi na kufanya kazi kwa bidii ili kutoa huduma iliyo bora.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza na watumishi wa Sekta ya afya wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi lililofanyika jijini hapa

Dkt. Ndugulile amesema anaamini kuwa Wizara ya Afya itafika mbali zaidi ikiwa watumishi watafanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuheshimiana bila kujali utofauti wa vyeo baina ya watumishi.

“Kila mmoja amuheshimu mwenzake kwa sababu ana mchango katika haya yote tunayoyafanya na tunategemeana sana kwenye kazi zetu za kila siku” amesema Dkt. Ndugulile.

Aidha, Dkt. Ndugulile amewataka watumishi kuziheshimu nafasi za uongozi walizonazo sasa kwa kuzienzi na kuhakikisha wanafanya kazi ili kuthibitisha kuwa kweli wanastahili kuwa kwenye nafasi hizo.

“Bado kuna watumishi wengine hawajajitafakari katika nafasi zao, lugha tunazozitoa, kutojituma, tuache kufanya kazi kwa mazoea” alisema Dkt. Ndugulile.

Awali akizungumza na wajumbe wa mkutano, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula amesisitiza watumishi kufanya kazi kwa umoja na kujitolea ili wote kwa pamoja kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Katika Mkutano huo wajumbe walipitia na kujadili masuala kadha wa kadha kuhusiana na Wizara ya Afya ikiwemo bajeti ya Wizara, mabadiliko ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii, Sera ya Afya, Bima ya Afya pamoja na masuala ya utendaji ndani na nje ya Wizara.

Mwisho
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com