Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Mji wa Mtukula wilayani Misenyi mkoa wa Kagera wakati akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya ardhi.
Sehemu ya wananchi wa Mji wa Mtukula wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya majalada ya ardhi aliyoyakuta katika ofisi ya halmashauri ya Misenyi mkoa wa Kagera wakati akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanali Denis Mwila na wa pili kushoto ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Elia Kamyanda na kulia ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi Misenyi Emanuel Samson.
Na Munir Shemweta, MISENYI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula amesema kuanzia sasa Mkuu wa Idara ya Ardhi atakayekutwa amekaa na hati
ya ardhi kwa muda mrefu bila kuipeleka ofisi ya Kamishna
Msaidizi wa Ardhi Kanda kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utolewaji hati
hiyo basi Mkuu huyo ataondolewa katika nafasi yake.
Dkt Mabula alisema hayo jana tarehe 15 Machi 2019 alipozungumza na
watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoani
Kagera akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali
kupitia sekta ya ardhi.
Kauli hiyo ya Dkt Mabula inafuatia kukuta baadhi ya hati katika
halmashauri ya wilaya ya Misenyi zikiwa kwenye masijala ya ardhi tangu mwaka
2017 bila kupelekwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Ziwa kwa ajili ya
kukamilishwa ili wahusika wapatiwe hati.
Alisema, baadhi ya halmashauri alizozitembelea wakati wa ziara
yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi
amebaini wakuu wengi wa idara ya ardhi wakiwa na hati kwenye ofisi zao kwa muda
mrefu bila kufanya jitihada zozote za kuhakikisha hati hizo zinaenda ofisi ya
Kamishna kwa ajili ya kukamilishwa ili wahusika wapatiwe hati.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, ucheleweshaji utoaji hati
miliki za viwanja na mashamba siyo tu unawakera wananchi bali unaikosesha
serikali mapato ya kodi ya ardhi kwa kuwa wananchi wanakuwa hawajamilikishwa
ardhi kwa mujibu wa sheria.
Dkt. Mabula ametoa onyo kali kwa Mkuu wa idara ya ardhi
halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoani Kagera kwa kukaa na hati kwa zaidi ya
miaka miwili kwenye ofisi yake bila kuwasilisha hati hizo ofisi ya
Kamishna Msaidizi Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kukamilishwa na hatimaye
kukabidhiwa kwa wahusika kwa haraka na wakati.
Katika hatua nyingine Dkt Mabula amewataka wananchi wa miji ya Kyaka na Mtukula
katika wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera kuchangamkia zoezi la urasimishaji
makazi holela ambalo limeonekana kusuasua katika miji hiyo.
Akizungumza na wakazi wa Kyaka na Mtukula kwa nyakati tofauti Dkt
Mabula alisema kuwa, haridhishwi kabisa na namna kasi ya urasimishaji
inavyoendelea katika miji hiyo ambapo takwimu zinaonesha wananchi waliojitokeza
kwenye zoezi hilo ni ndogo ukilinganisha na wakazi wa miji hiyo.
Dkt Mabula ametolea mfano wa Mji wa Mtukula katika kitongoji cha
Katede kuwa, pamoja na eneo hilo kuwa na Kaya 842 zenye wakazi zaidi ya 3000
lakini ni watu 13 tu waliolipia fedha za kurasimishiwa maeneo yao na watu hao
wamechangia jumla ya shilingi milioni moja na laki nane.
Aidha, Naibu Waziri Mabula amewataka wananchi wa miji ya Kyaka na
Mtukula kutofanya maendelezo katika eneo lolote ambalo hawajajua mipango yake
ili kuepuka kubomolewa na kupoteza haki zao kwa kujenga katika maeneo yasiyo
ruhusiwa ambapo ameitaka halmashauri ya wilaya ya Misenyi kupanga mpango wa
matumizi bora ya ardhi kwa lengo la kuwa na miji iliyopangika.
0 comments:
Post a Comment