NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuuchunguza ujenzi wa kibanda cha kuhifadhia jenereta ya kuvuta maji katika mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo mkoani Iringa kinachodaiwa kujengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 20.
Mbunge wa jimbo la kilolo vennance Mwamoto akimuelezea Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso juu ya mradi huo wa maji unavyoleta changamoto kwa wananchi wa jimbo la kilolo
Hichi ndio kibanda cha kuhifadhia jenereta ya kuvuta maji katika mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo mkoani Iringa kinachodaiwa kujengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 20.
NA FREDY MGUNDA,IRINGA
NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuuchunguza ujenzi wa
kibanda cha kuhifadhia jenereta ya kuvuta maji katika mradi wa maji wa Ruaha
Mbuyuni, wilayani Kilolo mkoani Iringa kinachodaiwa kujengwa kwa zaidi ya
Sh Milioni 20.
Aliyasema hayo juzi katika ziara yake ya siku moja
wilayani humo kukagua miradi mbalimbali ya maji, ikiwemo ile inayosuasua
kwasababu mbalimbali.
“Nimepata taarifa eti kibanda hiki kimejengwa kwa
zaidi ya Sh Milioni 20,” alisema na kuuliza ukweli wa taarifa hizo kwa mhandisi
wa maji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Enock Basyagire aliyesema hakuwepo
katika halmashauri hiyo wakati kikijengwa na kuomba akapitie nyaraka ili
kujiridhisha.
Aliwahimiza Takukuru kulifuatilia jambo hilo kwa
haraka na kama kutakuwa na kile alichoita “matumizi mabaya ya fedha za umma”
wahusika wakamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Wakati huo huo, waziri Aweso ameoneshwa
kusikitishwa kwake kuona katika mradi huo, tenki kubwa la kuhifadhi maji
limejengwa katika eneo lisilo na chanzo cha maji; ambalo kwa mujibu wa taarifa
ya mhandisi wa halmashauri hiyo, gharama yake ni zaidi ya Sh Milioni 45.
“Huu ni uhuni, mmejenga tenki la Sh Milioni 45 na
halijawahi kuwa na maji; mimi sio mtaalamu wa maji lakini najua, huwezi kujenga
tenki katika eneo lisilo na chanzo cha uhakika cha maji, ni bora hapa
mngechimba kisima kirefu huenda mngepata maji kwa ajili ya wananchi hawa wakati
mkisubiri mradi mkubwa,” alisema.
Akitoa onyo kwa wahandisi wa maji kuacha kucheza
na fedha za umma huku akiwataka wataalamu wa maji kutoka Bonde la Rufiji
kufanya utafiti kujua eneo linaloweza kuwa na maji yatakayonusuru mradi huo
ambao utekelezaji wake ulianza awamu ya nne ya Dk Jakaya Kikwete, Aweso alisema:
“Serikali haipo tayari kuona wataalamu wanaotakiwa
kuwasaidia wananchi kupata maji, wanatengeneza mazingira ya kula fedha za umma.
Alimuita mhandisi huyo mbele ya wananchi
waliokuwepo wakati akikagua tenki hilo na kumtaka kuwaomba radhi kwa ujenzi huo
ulioshindwa kuzingatia mambo ya kitaalamu; ombi lililopokelewa vizuri na
wananchi hao.
Katika kukabiliana na changamoto za matumizi
mabaya ya fedha za miradi ya maji inayosimamiwa na halmashauri, alisema Wizara
imeamua kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini hatua inayotarajiwa kusaidia
kukomesha tabia hiyo.
Alisema wakala hiyo itakapoanza itasaidia
kupunguza au kumaliza ulaji wa fedha za miradi ya maji na wahandisi wasio na
nia njema katika kushughulikia kwa weledi changamoto za maji katika maeneo yao,
wataondolewa na nafasi zao watapewa wengine.
Awali Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto
alimwambia naibu waziri huyo kwamba kata ya Ruaha Mbuyuni ni moja ya maeneo
yenye changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama katika
jimbo hilo.
Mwamoto alisema ukosefu wa maji safi na salama
katika kata hiyo umewaweka wananchi wake katika mazingira hatari ya kupata
magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipundupindu ambacho hutokea mara kwa mara.
“Leo umekuja mwenyewe, umejionea na umesikia
kutoka kwa baadhi ya wananchi, naomba uwaondoe hofu wananchi hawa,” alisema
huku naibu waziri akiahidi kuishughulikia changamoto hiyo kwa kasi kubwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruaha Mbuyuni, Adam
Danando alisema sehemu kubwa ya wananchi wa kijiji na kata hiyo wamekuwa
wakitegemea maji ya bonde la mto Lukosi yenye chumvi na bakteria ambao ni
hatari kwa afya zao.
0 comments:
Post a Comment