Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Wilaya ya Same imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwa Wilaya namba moja nchini kwa uzalishaji wa zao la Tangawizi huku Wilaya zingine Mkoani Kilimanjaro na nchi nzima kwa ujumla zikisalia kujifunza kupitia Wilaya hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe Rosemary Staki Senyamule mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe Mecky Sadick Juu wakati wa dhifa ya kukabidhi Cheti cha usajiri wa Kampuni mpya inayojihusisha na zao la Tangawizi ya Mamba Ginger Growers Company Limited.
Dc Staki alisema kuwa Ni furaha kuona hatua mpya ambazo kila siku zinaandaliwa zinazopelekea kukua kwa Mnyororo wa thamani (Value Chain) ya zao la Tangawizi.
"Tunao wajibu wa kuhakikisha tunabaki kuwa wazalishaji namba moja kwa ubora wa tangawizi Tanzania" Alisema Dc Senyamule
Amebainisha kuwa jambo hilo linahitaji mipango madhubuti na dhamira ya dhati ya kukuza zao hilo kwa kuzingatia weledi wa kilimo cha zao hilo sambamba na kanuni bora za kilimo.
Kampuni ya Mamba Ginger Growers Company Limited
imeanzishwa na chama cha ushirika ili kuingia mikataba na wadau watakaojitokeza kuwekeza katika uendelezaji wa zao la tangawizi ikiwa ni pamoja na viwanda vya kusindika tangawizi.
Dc Senyamule pia amesema kuwa katika dhifa hiyo kumeanzishwa jukwaa la Tangawizi linalohusisha wadau wa zao hilo la Tangawizi ambao watakuwa na kazi mahususi ya kujadili juu ya uendelezaji wa zao la Tangawizi.
Mhe Senyamule alisema kuwa Wilaya ya Same imejipanga kuhakikisha zao la Tangawizi linaongeza thamani na kuinua uchumi wa wananchi.
0 comments:
Post a Comment