Mwanafunzi kutoka Shule ya Kata Nkololo aliyefanya vizuri kwa kupata daraja la kwanza (pointi saba) na kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018 Ibrahimu Buyungumya(kushoto) na Mwanafunzi wa Kike Kwandu Maduhu kutoka Shule ya Sekondari Biashara aliyefanya vizuri kwa kupata daraja la kwanza (pointi 11) katika mtihani huo na kuongoza kimkoa (wasichana), wakionesha kadi zao za akaunti ambazo wamekabidhiwa (katika hafla maalum ya kuwapongeza iliyofanyika shule ya Sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari13, 2019 ) baada ya kufunguliwa akaunti na kuwekewa zawadi hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akiteta jambo na Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju, wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2018 iliyofanyika kimkoa, katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kushoto) akiwakabidhi zawadi ya ngao viongozi wa Halmashauri ya mji wa Bariadi ambayo iliongoza kimkoa na kushika nafasi ya tisa kati ya halmashauri zaidi ya 185 nchini katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018, (kushoto na wa pili kushoto) ni wanafunzi walifanya vizuri Kimkoa kutoka shule za Serikali), wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani huo iliyofanyika kimkoa katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa nne kushoto mbele) katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa na Halmashauri ya Mji wa Bariadi , walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, wanafunzi walawili walioongoza katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2018 Kimkoa na wazazi wao, baada ya hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani huo iliyofanyika kimkoa katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Wanafunzi wa shule za Serikali (kata) Wilayani
Bariadi, Ibrahim Buyungumya kutoka Shule ya Sekondari Nkololo , aliyepata
daraja la kwanza alama (points) saba na Kwandu Maduhu wa Biashara
Sekondari aliyepata daraja la kwanza alama kumi na moja, wamekiri kuwa kambi za
kitaaluma zimechangia kuongeza ufaulu wao katika Mtihani wa Kidato cha
Nne mwaka 2018.
Wanafunzi hao wameyasema hayo katika hafla ya
kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Matokeo
ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018 Kimkoa na kuufanya mkoa
kushika nafasi ya Tisa Kitaifa, iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Nkololo
wilayani Bariadi, Februari 13, 2019.
Wanafunzi hao wamesema pamoja na kumuomba Mungu,
juhudi zao binafsi za kujisomea, jitihada za walimu, malezi kutoka kwa wazazi
wanakiri kambi za kitaaluma zilizofanyika mkoani Simiyu kwa madarasa yote ya
mitihani ziliwasaidia kuwaandaa na mtihani huo wa Taifa, huku wakisisitiza
kambi hizo ziwe endelevu na wakapendekeza kuwa kwa mwaka 2019 ziongezewe
muda na zianze mapema zaidi.
“ Namshukuru Mungu kunifanikisha kupata daraja la
kwanza alama saba, nawashukuru walimu wangu, wazazi wangu kwa namna walivyokuwa
msaada kwangu; pia kipekee namshukuru Mkuu wetu wa Mkoa kwa kutuletea
kambi, zimetusaidia sana maana tulipata nafasi ya kukutana na wanafunzi
wenzetu na walimu mahiri kutoka shule mbalimbali na zilitusaidia kuelewa masomo
kwa mawanda mapana zaidi” alisema Ibrahimu Buyungumya.
“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata daraja la
kwanza alama 11, nawashukuru wazazi, walimu pia nashukuru uwepo wa kambi za
kitaaluma ambazo zilitusaidia sana kujiandaa vema na mtihani wetu, nashauri
kambi hizi zianze mapema na muda uongezwe ili ziwasaidie wadogo zetu
wafaulu vizuri zaidi yetu sisi” alisema Kwandu Maduhu.
Mkuu wa Shule ya sekondari Biashara, Mwl. Mathias
Joseph ambaye shule yake ilifanya vzuri kwa kupata alama A 23 na alama B 79
amesema pamoja na kambi za kitaaluma siri nyingine ya kufanya vizuri ni
jitihada zilizofanywa na walimu pamoja na usimamizi mzuri wa mikakati
iliyowekwa na idara ya Elimu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi,
ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi na mitihani ya mara kwa mara.
Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza walimu
waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Matokeo ya mtihani wa
Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018 katika mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka amewapongeza viongozi, walimu, wanafunzi, wazazi na
wadau wote wa elimu mkoani humo, kwa jitihada walizofanya katika kuongeza
ufaulu.
Aidha, Mtaka ameelekeza kamati zote za shule
zikutane na wazazi wa wanafunzi wa madarasa ya mtihani ili wakubaliane juu ya
wanafunzi hao kuanza kambi za kitaaluma na wazazi hao wachangie chakula ambacho
watoto wao wangekula wakiwa majumbani kwao kitumike wakiwa kambini.
“Nilishatoa maelekezo na nayarudia; kamati za shule
zikae na wazazi wakubaliane madarasa yote ya mtihani watoto waanze kambi za
kitaaluma na wazazi wachangie chakula kile kile ambacho watoto wangekula wakiwa
nyumbani, ili watoto wapate nafasi nzuri ya kusoma na kujiandaa na mtihani wa
Taifa” alisema Mtaka.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa
wa Simiyu, Enock Yakobo ametoa wito kwa wazazi mkoani humo kuhimiza
watoto kusoma ili waweze kufikia ndoto zao akakemea tabia ya baadhi ya wazazi
kuwaachisha masomo watoto wa kike na kuwaozesha.
Jumla ya wanafunzi 7094 kati yao wavulana ni 4224
na wasichana 2875 walifanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2018
mkoani Simiyu na kuwezesha mkoa kushika nafasi ya tisa Kitaifa kati ya mikoa
31, ambapo umepanda kwa nafasi mbili ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo
ulishika nafasi ya 11 Kitaifa.
Katika pongezi zilizotolewa kwa walimu na wanafunzi
mwanafunzi wa kiume aliyeongoza Kimkoa amezawadiwa shilingi milioni Moja,
mwanafunzi bora wa kike shilingi laki tano (wote wamefunguliwa akaunti)
na kuahidiwa kupewa mahitaji yote muhimu watakapochaguliwa kidato cha tano,
huku walimu sitini kila mwalimu akipewa shilingi elfu ishirini kwa kila
alama A iliyopatikana kwenye somo lake.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment