METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 9, 2018

WIZARA YA MADINI, SUMA JKT WASAINI MIKATABA YA UJENZI VITUO VYA UMAHIRI




Na Asteria Muhozya, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT, Mhandisi Morgan Nyonyi wamesaini Mikataba Mitatu ya kuanza ujenzi wa Vituo Saba vya Umahiri pamoja na Jengo la Mafunzo kwa Wachimbaji wadogo katika Chuo Cha Madini, Dodoma.

Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo imefanyika leo tarehe 9 Julai, 2018, Makao Makuu ya Wizara ya Madini jijini Dodoma na kushuhudiwa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Akizungumza baada ya utiaji saini, Waziri  Kairuki amesema kuwa, tukio hilo ni utekelezaji wa  ahadi aliyoitoa wakati akiwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 ambapo alieleza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini itaanza ujenzi wa ofisi saba za madini ili zitumike kama vituo vya umahiri vya  masuala ya madini.

Waziri Kairuki amezitaja ofisi hizo kuwa ni Mpanda, Songea, Chunya, Tanga, bariadi, Bukoba na Musoma na kuongeza kuwa, ni pamoja na upanuzi wa miundombinu ya Chuo Cha Madini Dodoma kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za madini zinazotekelezwa na Chama Cha Wachimbaji Madini Wanawake.

“ Ujenzi wa Vituo hivyo unatekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ambapo moja ya malengo mahususi ya mradi huu ni kuboresha Sekta ya madini nchini hususan kuwasaidia wachimbaji wadogo ili kuwaongezea ujuzi katika eneo la uchimbaji wa madini na kukuza uchumi,” amesisitiza Kairuki.

Akizungumzia umuhimu wa vituo hivyo, alisema vimelenga katika kutoa mafunzo ya jiolojia hususan katika utafiti wa madini, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususan zisizotumia kemikali ya Zebaki.

Ameongeza kuwa, vituo hivyo pia vitatoa mafunzo ya biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo wa madini, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo ya namna bora za utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji wadogo.

Kuhusu gharama za ujenzi wa vituo hivyo amesema kuwa ujenzi wake utagharimu jumla ya shilingi Bilioni 11.9.

Akizungumzia sababu za kuingia Mkataba na SUMA JKT, Waziri Kairuki amesema kuwa, jeshi hilo limekuwa likijihusisha na kazi mbalimbali  za ujenzi, kujiimarisha kwao nchini, uwezo wao kiufundi katika kutekeleza miradi mikubwa, gharama nafuu, ubora na kuongeza kuwa, mkataba na SUMA JKT utaokoa kiasi cha shilingi milioni 249.3 ikilinganisshwa na wakandarasi wengine.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Msanjila amesema kuwa, ujenzi wa vituo hivyo umelenga kuwasaidia wananchi na zaidi ukilenga wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT, Mhandisi Morgan Nyonyi amesema kuwa, Jeshi hilo limejipanga kutekeleza mradi huo ndani ya muda uliopangwa wa kipindi cha miezi sita   na utekelezaji wake utafanywa kwa weledi.

Kazi ya ujenzi wa vituo hivyo itasimamiwa na washauri Elekezi  Kampuni ya Y & P Architects ambayo imesanifu majengo ya  Chuo Cha Madini Dodoma na Kampuni ya Interconsult Ltd ambayo imesanifu majengo ya Musoma, Bariadi na Bukoba.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com