Na Stella
Kalinga, Simiyu
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini Marco Mtunga
amewaonya wanunuzi wa Pamba watakaonunua pamba nje ya mfumo wa Vyama vya
Ushirika vya Msingi (AMCOS) na kuwa endapo watabainika Pamba hiyo itataifishwa
na Serikali.
Onyo hilo limetolewa Mkoani Simiyu katika kikao baina
ya Viongozi wa mkoa huo, viongozi wa vyama vya ushirika vya Msingi (AMCOS),
wanunuzi wa Pamba na Naibu Mrajisi
kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dodoma Charles Malunde, lengo
likiwa ni kukumbusha juu ya uadilifu katika masuala ya ununuzi wa pamba, ikiwa
ni maandalizi wa ununuzi pamba baada ya msimu kufunguliwa.
Mtunga amesema
mwaka huu Serikali imefanya uamuzi kwamba pamba yote itakayozalishwa hapa
nchini itanunuliwa kupitia Vyama vya Msingi (AMCOS) jambo ambalo amesema
limeelezwa vizuri katika mwongozo wa bodi.
“Tunawatahadharisha
wanunuzi wa pamba kufuata mfumo wa ununuzi wa pamba uliowekwa na Serikali,
pamba yote itakayokamatwa ikiwa haikununuliwa kupitia Chama cha Ushirika cha
Msingi itataifishwa na Serikali, katika
mwongozo tulioutoa maelekezo hayo yapo na yako chini ya sheria Namba 2 ya pamba
ya mwaka 2001” alisema Mtunga.
Kwa upande wake
Naibu Mrajisi kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dodoma Charles Malunde
amewataka viongozi wa Vyama vya ushirika kuepuka aina yoyote ya wizi na
ubadhilifu wa kutumia udanganyifu wa kuwaibia wakulima kwa kuziharibu mizania.
Aidha, Malunde
amesisitiza sheria na taratibu za Ushirika zizingatiwe katika uendeshaji wa
Vyama vya Ushirika vya Msingi, hivyo akawataka viongozi wote waliochaguliwa
kuongoza vyama hivyo ambao wana shutuma zozote, watumishi wa Umma au Viongozi
wa Serikali na Vyama vya Siasa kuachia mara moja nafasi hizo kwa kuwa hawana
sifa kwa mujibu wa sheria.
Baadhi ya viongozi
wa AMCOS waliwasilisha masuala mbalimbali kama maombi yao kwa Serikali
kuhusiana na ununuzi wa pamba ikiwa ni pamoja na kuomba vyama vya ushirika vya
msingi vipya vilivyo katika hatua ya
usajili vikamilishiwe usajili ili viweze kuingia katika mfumo huu wa ununuzi wa
pamba.
Akihitimisha kikao
hicho Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema anatamani kuona ushirika wenye
mtazamo wa kujibu changamoto na mahitaji ya wakulima wa pamba, huku akitoa
angalizo kwa viongozi wa AMCOS watakaofanya ubadhilifu wa fedha za Vyama vya Ushirika
kuwa Serikali mkoani humo itawachukulia hatua kali.
“Ushirika wa
Simiyu (is my own baby) ni mtoto wangu mwenyewe, ni kitu ambacho nilitamani
kuona kinatokea, Wanaushirika wakakaokosa uadilifu wajihesabu kuwa wafungwa
watarajiwa, nawaambia nitawafunga na sitanii nitawafunga” alisisitiza Mtaka.
Katika hatua
nyingine amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuaandaa eneo la
ujenzi wa Makao Makuu ya Chama Kikuu cha Ushirika Simiyu.
0 comments:
Post a Comment