Na
Stella Kalinga, Simiyu
Mwalimu Akwilina Ernest Marenge
kutoka Shule ya Msingi Salunda katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani
Simiyu, amepata zawadi ya shilingi 500,000/= kwa ajili ya pongezi kwa
kufanikiwa kutoa Alama A kwa wanafunzi 90 kati ya wanafunzi 147 katika Somo la
Kiswahili katika mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2017.
Fedha hizo zimetolewa na Mkuu wa
Mkoa wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa mwalimu huyo mbele ya baadhi ya
viongozi wa mkoa huo, wanafunzi na walimu wengine wa Shule ya Msingi
Salunda.
Akikabidhi fedha hizo Mtaka amesema Serikali imetambua
juhudi za mwalimu huyo ambaye Katika
somo lake la Kiswahili alikuwa na ufaulu mzuri ambapo alitoa alama A 90, Alama
B 55 na Alama C 2, hivyo
kama kiongozi ameona ni vema mwalimu huyu akapewa motisha.
"Siku ya Mei Mosi alipewa
shilingi laki tano kama mfanyakazi hodari na mimi nikasema nitampa shilingi
500,000 za kwangu siyo za Serikali, kama kiongozi niliona ni jambo la
kupongezwa, Fedha hii haifanani na alichofanya kwa watoto ila najua wanafunzi
wake watamkumbuka daima" alisema Mtaka.
Kwa upande wake Mwl. Akwilina
Marenge ambaye anatarajia kustaafu mwezi Juni mwaka 2018 amemshukuru Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa kutambua juhudi zake na kuona umuhimu wa
kumpongeza na akatoa wito kwa walimu wengine kujituma na kupenda kazi yao.
Nao Walimu wenzake na Mwalimu
Akwilina wamempongeza na kubainisha kuwa anastahili kupata zawadi zote
hizo kwa kuwa pamoja na kuwa umri mkubwa amekuwa ni mtu wa kujituma na
kufanya kazi kwa bidii zaidi ya walimu vijana.
"Mwalimu Akwilina ni mwalimu wa
tofauti na walimu wengine, pamoja na kwamba yeye umri wake umekwenda sana
anawahi kazini, anaipenda kazi yake, anajituma kuliko hata walimu vijana, ni
mcheshi; hata sasa hivi tunavyosikia anaenda kustaafu tunasikitika kwa sababu
anaondoka mtu mchapakazi" alisema mwalimu Tabitha Erasto.
" Huyu mama ni mtu mzima lakini
anajituma kuliko baadhi ya walimu vijana ni kitu cha kushangaza mno, japo
anaelekea kustaafu sisi wenzake tunaobaki tunapaswa tuige mfano wake kwa
kweli" Alisema Mwalimu Joyce Mishana.
Akitoa shukrani kwa niaba ya walimu
wengine Mwalimu Mkuu wa Shule ya Salunda, Mwl. Nchambi Tupendane amemshukuru
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa kutambua mchango wa mwalimu Akwilina na kubainisha
kuwa zawadi hiyo imekuwa ni chachu kwao ya kufanya vizuri zaidi katika Mtihani
wa Taifa mwaka huu na miaka ijayo.
Kutokana na utendaji kazi mzuri
Mwalimu Akwilina pia alitambuliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi kuwa Mfanyakazi Hodari na siku ya Mei Mosi alizawadiwa shilingi
laki tano na cheti.
0 comments:
Post a Comment