METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, April 23, 2018

BARAZA LA WAFANYAKAZI (NFRA) LATUAMA KWA SIKU MBILI MJINI DODOMA


Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi NFRA, Bi Vumilia L. Zikankuba akifungua mkutano maalumu wa Baraza hilo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya biashara wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) akifatilia mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe wakifatilia mkutano huo.


Na Mathias Canal, NFRA-Dodoma

Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) limekutana kwa siku mbili Mjini Dodoma kwa ajili ya mkutano wake wa nane ambapo pamoja na mambo mengine kunajadiliwa taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa shughuli za wakala mwaka 2016/2017 na taarifa ya nusu mwaka 2017/2018 sambamba na mpango na bajeti ya mwaka 2018/2019.

Mkutano huo ulioanza jana 22 Aprili 2018 unaofanyika katika ukumbi wa mikutano NFRA Makao makuu uliopo Mtaa wa Relini-Kizota Manispaa ya Dodoma ni sehemu ya utimilifu na utekelezaji wa majukumu ya kiushauri sambamba na kujadili shughuli mbalimbali za wakala.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi NFRA, Bi Vumilia L. Zikankuba amewapongeza wajumbe wote kwa kushiriki mkutano huo huku akitoa heko kwao kwa kuwa sehemu ya ushiriki uliotukuka kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maghala na Vihenge vya kisasa (Silos) iliyofanyika Aprili 21, 2018.

Aliwasihi wajumbe kwa kauli moja kuwa na mshikamano kazini kwani kufanya hivyo kutaongeza chachu ya ufanisi katika kazi ikiwa ni pamoja na utendaji uliotukuka hivyo kupelekea utendaji mzuri wa wakala na serikali kwa ujumla wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya biashara wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA), Ndg Mikalu Mapunda, akiwasilisha taarifa ya nusu mwaka ya utekelezaji wa shughuli za wakala kwa mwaka 2017/2018 alisema kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi, uwezeshaji na usimikaji wa mifumo ya kielektroniki, Utawala bora na uwajibikaji.

Sambamba na mafanikio hayo pia amezitaja changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli za wakala ikiwa ni pamoja na kuchelewa kupokea fedha za ruzuku kutoka hazina, Ufinyu wa bajeti inayoidhinishwa kuuzwa kwa wakala kutofika, na baadhi ya mahindi yanayowasilishwa kwa wakala kutokidhi vigezo.

Mapunda alisisitiza kuwa wizara ya kilimo kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya ziendelee kuendesha mafunzo kuhusu uhifadhi bora wa nafaka baada ya uvunaji.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com