METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 4, 2018

HUU NDIO UJUMBE WALIOPEWA WANAUME WA KATA YA KITUNDA KATIKA BONANZA LILILOANDALIWA NA CDF

Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Ilala Joyce Maketa akiongea na waandishi wa habari mapema jana katika Bonanza lililoandaliwa na CDF kwa kushirikiana na ISDI.

Matokeo ya takwimu nyingi kwa sasa yanaonyesha kuwa maswala ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto yamepungua kwa asilimia kubwa  na hii ni  kutokana na serikali kuweka mikakati na mipango thabiti ya kudhibiti tatizo hili.

Hayo yamesemwa mapema jana jijini Dar es salaam na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Bi. Joyce Maketa wakati akiongea na wakazi wa kata ya Kitunda katika Bonanza la Uhamasishaji juu ya Majukumu ya Wanaume na wavulana katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Afisa huyo alisema kuwa kwa Manispaa ya Ilala kwa sasa matukio hayo yamepungua na ni kutokana na huduma zinazoendelea kutolewa pamoja na kuwepo na maafisa ustawi wa jamii wengi katika kata 16 na wasaidizi ambao ni zaidi ya 36 katika kata zote za wilaya nzima ya Ilala.

Aidha afisa huyo alisema kuwa amefurahishwa na bonanza hilo lililoandaliwa na CDF pamoja na ISDI kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswidi (SIDA) kwa kuweza kuwakutanisha vijana wa kiume na wanaume ili wawe mabalozi wazuri wa kutetea na kupigania haki za mtoto wa kike ambazo atazipoteza kama hatopewa ulinzi stahiki na jamii inayomzunguka.

Aliendelea kusema kuwa kwa muitikio huu inaonyesha kuwa wanaume kwa wanawake wapo tayari katika mapambano dhidi ya vitendo vyote visivyofaa katika jamii kama Ubakaji, Ulawiti, Ukeketaji na Ndoa pamoja na Mimba za utotoni na wamejiandaa ipasavyo kukabiliana na tatizo hilo.
Afisa Ushirikishaji Wanaume wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) Bw. Kiswigo Ibrahim Mwan`gonda akiongea na washiriki  kuhusu dhumuni la kongamano hilo mapema jana jijini Dar es salaam.

Kwa upende wake Afisa Ushirikishaji Wanaume wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) Bw. Kiswigo Ibrahim Mwan`gonda alisema kuwa lengo la bonanza hilo ni kuwakutanisha na kuwaunganisha wanaume kupitia michezo na kuwahakikisha wanaume wanapata ujumbe kuwa wao wanajukumu kubwa la kuhakikisha wanalinda na kuthamini haki za mtoto wa kike.

Aliendelea kusema kwa kuwa wanaume ni sehemu kubwa ya tatizo la ukatili wa kijinsia na ndio watekelezaji wakubwa wa ukatili huo wameamua kukaa nao ili kutafuta suruhisho la kudumu kuhusiana na tatizo hilo ili kuhakikisha watoto wakike wanaishi katika jamii yenye haki na usawa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ISDI Bw. Jonas Tiboroha akielezea kwa ufupi shughuli zinazofanywa na shirika hilo.

Meza kuu ikifuatilia matukio yanayoendelea katika Bonanza lililoandaliwa na shirika la CDF.

Mgeni Rasmi Joyce Maketa akikagua wachezaji kabla ya kuanza kwa mechi kati ya Waendesha Boda boda wa Kitunda na timu ya Kitunda United.

Wachezaji, wafanyakazi wa CDF na ISDI wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com