Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Bibi
Florence Max Mambali wakati alipotembelea banda la Kampuni ya kufuga
kuku na kuzalisha vifaranga vya kuku ya Mkuza Chicks katika
Maonesho ya Viwanda Mkoa wa Pwani yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Sabasaba
uliopo katika eneo la Picha ya Ndege, Kibaha, Oktoba 3, 2018. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu)
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa
amezitaka Wizara zinazohusika na masuala ya viwanda, Ofisi za Wakuu wa Mikoa,
Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na sekta binafsi watambue na
waondoe vikwazo na urasimu dhidi ya ujenzi na ustawi wa viwanda nchini.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ampelekee taarifa ya
hatua iliyofikiwa juu ya kampuni ya Budget Motors walioomba kibali cha
kutengeneza na kuunganisha bodi za mabasi tangu mwaka jana na hawajajibiwa.
Waziri Mkuu ametoa agizo
hilo leo (Jumamosi, Novemba 3, 2018) wakati akifunga wiki ya maonesho ya
viwanda yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba katika kata ya Picha ya
Ndege, Kibaha mkoani Pwani. Amesena uwepo wa viwanda nchini unatoa ajira
nyingi.
“Serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeamua kujenga uchumi wa viwanda
utakaokuwa mhimili mkuu wa maendeleo ya Taifa na wananchi, hivyo itaendelea
kutoa ushirikiano ili kuhakikisha ajenda ya ujenzi wa viwanda inafanikiwa.”
Amesema katika kupunguza
vikwazo na kuboresha sera nchini, Rais Dkt. Magufuli ameweka msukumo wa kutosha
ili kurahisisha na kuondoa ukiritimba kwenye shughuli zote za kibiashara,
lakini pia katika kuboresha sera za Taifa za kodi ili kulinda viwanda vya ndani
Waziri Mkuu amesema umuhimu
wa viwanda umetokana na Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka
2015/2020 ambayo inaielekeza Serikali kuweka nguvu katika ujenzi wa viwanda ili
kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.
Amesema kwa msingi huo,
Rais Dkt. Magufuli alitoa msukumo wa sekta binafsi nchini kuanzisha viwanda
vinavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini kutokana na mazao ya kilimo,
mifugo, uvuvi na maliasili, vikiwemo viwanda vya nguo, sabuni, korosho na
matunda.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa
uwepo wa viwanda nchini utasaidia kuongeza wigo wa mapato ya Serikali kupitia
kodi na tozo mbalimbali. “Huu ndio mwelekeo wa Serikali ya awamu ya tano
unaolenga kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.”
Kuhusu suala la kampuni ya
Budget Motors, Wiziri Mkuu amesema ifikapo Ijimaa (Novemba 9, 2018) Waziri wa
Viwanda Biashara na Uwekezaji awasilishe taarifa kuhusu suala hilo la kibali.
“Huu ni urasimu, ni bora apewe atengeneze na akikosea arekebishwe.”
Kampuni ya Budget Motors
inadai kuwa iliomba kibali cha kuwa na uthibitisho wa kutengeneza na
kuunganisha bodi za mabasi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa
takribani mwaka mmoja bila ya kujibiwa. Walitoa malalamiko hayo kwa Waziri Mkuu
alipotembelea banda lao.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa rai kwa taasisi zenye miradi mbalimbali nchini
pamoja na wananchi kuthamini na kuzitumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya
hapa nchini zikiwemo na za viwanda vya mkoa wa Pwani kwani zina viwango vya ubora.
“Wakati natembelea mabanda
kwenye maonesho haya nimeshuhudia bidhaa nyingi nzuri na zenye ubora. Nimeona
wazalishaji wa saruji, mabati, nondo, marumaru, mabomba ya plastiki, chuma,
zana za kilimo, vyakula, vinywaji na vifungashio.”
Waziri Mkuu amesema kupitia
maonesho hayo ya viwanda vilivyopo katika mkoa wa Pwani vimeudhihirishia umma
kuwa vina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa zilizo bora na hata kuzidi zile
zinazoingizwa kutoka nje, amewahamasisha wananchi kutumia bidhaa za ndani.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo ameiagiza mikoa
yote nchini kuhakikisha inatumia bidhaa zinatengenezwa na viwanda vya ndani
katika miradi mbalimbali ya ujenzi wanayoitekeleza kama ujenzi wa hospitali za
wilaya na vituo vya afya.
Amesema Wakuu wa Mikoa ni
lazima wahakikishe bidhaa kama saruji, nondo, marumaru, mabati zinavyotumika
katika ujenzi ziwe vimezalishwa na viwanda vya ndani kwa sababu vina viwango
vya ubora unaotakiwa na pia itasaidia kuondoa tatizo la soko la bidhaa hizo.
Naye,Waziri Mwijage amewataka watendaji wanaohusika na masuala ya viwanda
kutoweka vikwazo kwa wawekezaji ambao wanakwenda katika ofisi zao kwa ajili ya
kutafuta maeneo ya kuwekeza kwenye viwanda au wanaohitaji vibali kwani jambo
hilo halina tija.
0 comments:
Post a Comment