METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, December 13, 2017

KAKUNDA AKOSHWA NA MIRADI YA TABIANCHI NA ARUSHA JIJI

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Joseph Kakunda akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wilayani Longiod na baadhi ya Maafisa kutoka OR TAMISEMI, Mkoa Arusha na Wilaya ya Longido wakati wa ziara yake ya kikazi
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Joseph Kakunda akiwa na mtoto wa kisonjo mbele ya boma lao (nymba) aliposhuka kuwasalimia wananchi wakati wa ziara yake alipokwenda kukagua mradi wa maji kuanzia chanzo chake Oldonyo Sambu wilayani Longido. Mwenye kofia ni Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Rashid Taka
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Joseph Kakunda akipatiwa maelezo na Mkuu wa Wilaya ya Monduli kuhusu mradi wa maji unaotekelezwa na IIED na Haki Kazi Catalyst katika kijiji cha Engaruka. Maji hayo wanatumia binadamu na wanyama pori mbalimbali.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Joseph Kakunda amewataka Wahandisi kujifunza utekelezaji wa kazi zinazotekelezwa na Miradi ya Tabia nchi (Decentralized Climate Change) mkoani Arusha.

Akiongea na Waandishi wa Habari katika ofisi za Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, wakati wa majumuisho yake ya ziara ya kikazi aliyoimaliza mkoani Arusha hapo jana, Mhe. Kakunda amesema ameridhishwa na Miradi ya maji ya Halmashauri ya Jiji la Arusha na ile ya Tabia nchi inayotekelezwa na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ‘IIED’ ya Uingereza.

“Nimeridhishwa na viwango vya utekelezaji wa miradi ya maji ya Jiji la Arusha, kwa hiyo ndugu zangu mimi nafurahi, kwa kazi ambazo nimeziona hapa Arusha, hii ni wazi kwa Watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inajitahidi katika kutekeleza kazi mbalimbali za maendeleo”

Mhe. Kakunda ametoa agizo kwa Jiji la Arusha kuwa, chanzo cha maji kilichopo eneo la Ngaramtoni na Magereza vichunguzwe na kulindwa, kwani ndio vyanzo vya uhakika wa maji ambavyo vitaweza kufanya tatizo la maji Jijini Arusha kuwa historia.

 “napenda kutoa agizo kwa Jiji la Arusha, kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji vipimwe, vipimwe na vilindwe” pia amewataka katika vyanzo hivyo viingizwe katika mpango mkuu wa Jiji hilo ‘master plan’

Aidha, amewataka wananchi kuupokea Mradi wa maji wa Jiji hilo unaotekelezwa hivi sasa, kama mradi wa Serikali na kwamba Serikali haitawaacha. Mradi huo mkubwa ulianza katika mwaka wa fedha 2016/2017 chini ya Mamlaka ya Maji safi na maji taka Arusha (AUWSA), ukiwa unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na umepata mkopo wa masharti nafuu wa shilingi Bilioni 476 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).

Katika hatua nyingine, Mhe. Kakunda ameipongeza Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza ‘IIED’ na Haki Kazi Catalyst wanaotekeleza Miradi ya mabadiliko ya Tabia nchi mkoani Arusha na kwamba ni fursa kwa wahandisi kwenda kujifunza na kujitathmini.

Amewasisitiza Wahandisi wajitathmini kufanya miradi yao kuwa na bei nafuu kama ilivyo kwa miradi ya tabia nchi iliyopo Monduli, Longido na Ngorongoro mkoani Arusha ambayo michakato yake hadi kukamilika inatumia fedha kidogo.

“natoa wito kwa Wahandisi wote wa maji, wa Wizara ya maji na TAMISEMI, Wahandisi walioko mikoani na Katika Mamlaka zetu, waende wakajifunze katika Miradi ya maji ya Mabadiliko ya Tabia nchi, watajifunza ni kwa nini hawa wenzetu wameanzisha (design) miradi ya bei nafuu, miradi ya milioni 80 hadi 100 na inahudumia watu 4,000 hadi 5,000 au 6,000 ni kwanini miradi yetu ambayo ni kama hiyo hiyo inagharimu hadi milioni 500”

Pia Mhe. Kakunda amewataka wananchi wote wenye visima vya maji Jijini Arusha na mkoani humo, kwenda kupima maji yao katika maabara kwa lengo ya kuyachunguza kabla ya kuyatumia kwani yanaweza kuwa na madhara kwa afya zao na mifugo jambo ambalo ni muhimu kulifanyia kazi mapema.

Mhe. Kakunda amemaliza ziara yake ambayo aliianza mkoani Kilimanjaro na kuhitimisha katika mkoa wa Arusha.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com