Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
MAJI ni hitaji muhimu sana katika
uhai wa mwanadamu na viumbe wengine na ndiyo maana Maendeleo ya kiuchumi
ya nchi yoyote duniani yawe ya viwanda, kilimo na kadhalika yanategemea
maji.
Lengo namba sita la Malengo
Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2015-2030 linaweka msisitizo wa
upatikanaji wa huduma za maji safi na salama na usafi wa mazingira kwa
wote ikienda sambamba na ulinzi wa rasilimali za maji na miundombinu ya
usambazaji maji.
Wakati mahitaji ya maji
yanaongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu na kukua kwa shughuli
za kiuchumi na kijamii, maeneo kame yameendelea kuwa kame zaidi na
matukio ya mafuriko yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Inaelezwa kuwa zaidi ya watu
bilioni 2.1 duniani hawapati maji safi na salama na kati ya hao, watu
milioni 844 hawapati huduma za msingi za maji ya kunywa, ambapo kati yao
zaidi ya watu milioni 340 wanatoka katika Bara la Afrika.
Hali hiyo inaonesha jitihada zaidi
zinahitajika katika kuwekeza na kuendesha mindombinu ya huduma za maji
kwa ajili ya kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma za majisafi na
usafi wa mazingira ili kuendana na kasi ya mahitaji ya maji na malengo
ya nchi na ya Umoja wa Mataifa.
Katika Tanzania mahitaji ya maji
kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile majumbani, umwagiliaji,
viwanda na mazingira ni wastani wa mita za ujazo bilioni 40 kwa mwaka
kati ya mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka zilizopo.
Aidha makadirio yameonesha kuwa
mahitaji ya maji yataongezeka kufikia wastani wa mita za ujazo bilioni
57 kwa mwaka ifikapo mwaka 2035 na kutokana na mwenendo wa kuongezeka
kwa mahitaji ya maji nchini, Serikali imeimarisha ulinzi wa rasilimali
za maji ili kulifanya Taifa lisikumbwe na uhaba wa maji katika siku za
usoni katika maeneo ya mijini na vijijini.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio
ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Maji
Prof. Makame Mbarawa anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali imeendelea kutekeleza miradi ya maji mijini na vijijini kwa
kujenga miradi mipya, kukarabati na kupanua miradi iliyopo kwa kutumia
vyanzo vya maji vya visima virefu na vifupi, mabwawa, chemchemi, mito na
maziwa.
Prof. Mbarawa anasema katika
kipindi cha mwezi Julai 2018 hadi mwezi Desemba 2018, jumla ya miradi
198 yenye vituo vya kuchotea maji 4,719 imekamilika na kuwanufaisha
wananchi wapatao 1,252,731 waishio vijijini na miradi 653 inaendelea
kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Waziri Mbarawa anasema Serikali
inaendelea na ujenzi wa miradi ya maji vijijini pamoja na kutekeleza
programu mbalimbali za kuimarisha uendeshaji na matengenezo ya miradi
hiyo ili iwe endelevu ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maji katika
vijiji 77 iliyofikia katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
“Katika mwaka 2018/2019, Serikali
kwa kushirikiana na BADEA, OFID, Saudi Fund na Kuwait Fund inatekeleza
mradi wa maji Same-Mwanga–Korogwe wenye lengo la kuwapatia huduma ya
maji wakazi wa miji ya Same na Mwanga, pamoja na vijiji 38 vilivyopo
kandokando ya bomba kuu katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe”
anasema Waziri Mbarawa.
Anaongeza kuwa mradi huo
unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusu ujenzi wa
miundombinu ya uzalishaji maji pamoja na miundombinu ya kusambaza maji
katika miji ya Same, Mwanga na vijiji tisa vilivyopo kandokando ya bomba
kuu na awamu ya pili itahusu kusambaza maji katika vijiji 29
vilivyobaki ambapo Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya
kuanza utekelezaji wa awamu hiyo.
Akifafanua zaidi Prof. Mbarawa
anaongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi umegawanywa katika vipande
vinne, kipande cha kwanza kilichogharimu Dola za Marekani Milioni 41.36
kinahusu ujenzi wa miundombinu ya kuzalisha maji, ulazaji wa bomba kuu
la kusafirisha maji hadi kwenye tanki la kuhifadhia maji, mtambo wa
kusafisha maji pamoja na ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji.
Prof. Mbarawa anasema kuwa
Serikali pia inatekeleza utekelezaji wa mradi wa maji wa Masoko uliopo
Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya ambao unahusisha ulazaji wa mtandao wa
mabomba, ujenzi 50 wa vidakio vya maji, matanki ya maji na vituo vya
kuchotea maji. Hatua za utekelezaji wa mradi zimegawanyika katika
vipande vitano.
“Mradi wa maji Masoko
utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 wanaoishi katika
vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi,
Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na
Nsanga”.
Aidha Ppof. Mbarawa anasema mradi
wa maji wa vijiji 100 vilivyopo kandokando ya bomba kuu la maji kutoka
Ziwa Victoria hadi miji ya Kahama na Shinyanga unaendelea kutekelezwa
chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Kahama – Shinyanga
(KASHWASA), ambapo wamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo
itahusisha vijiji 40 ambapo vijiji 33 vimefanyiwa usanifu.
Anaongeza kuwa kati ya vijiji
vilivyofanyiwa usanifu, ujenzi wa miradi kwenye vijiji 14 umekamilika na
kunufaisha wananchi wapatao 38,348. Vijiji hivyo ni Runele, Gatuli,
Nyashimbi, Magobeko, Kakulu, Butegwa, Nyang’homango, Ng’homango,
Jimondoli, Kadoto, Lyabusalu, Mwajiji, Ichongo na Bukamba.
Kuhusu mradi wa maji wa Chiwambo
uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi uliogharimu Shilingi
bilioni 4.49, ulikamilika mwezi Mei, 2018 ambapo unahudumia vijiji
vijiji 30 vilivyopo Kata za Lulindi, Lupumbulu, Namalenga, Chiungutwa,
Sindano, Mchauru na Mbuyuni na utekelezaji wa mradi huo ulihusisha
ukarabati wa matanki na miundombinu ya maji iliyochakaa, ujenzi wa
matanki ya kuhifadhi maji.
Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa
anasema Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliunda Timu
ya Wataalam kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa kina wa mradi wa
maji Ntomoko uliopo katika vijiji vya Ntomoko-Fai na Makirinya
Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma pamoja na vijiji vya
Kinkima na Lusangi vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
Anasema ili kuteleza mradi huo
mwezi Februari mwaka huu, Serikali ilisaini mkataba wenye thamani ya Tsh
Bilioni 2.27 na Mkandarasi tayari ameanza maandalizi ya utekelezaji wa
mradi huo ikiwa na pamoja na ujenzi wa matanki matatu, ununuzi wa pampu,
ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji pamoja na ujenzi wa chemba.
Serikali inaendelea kutekeleza
miradi mikubwa ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo itihada
zaidi zinahitajika katika kuwekeza na kuendesha mindombinu ya huduma za
maji kwa ajili ya kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma za majisafi
nchini.
0 comments:
Post a Comment