METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, November 9, 2017

DKT MWANJELWA: SERIKALI KUFANIKISHA UWEPO WA SOKO LA BIDHAA (COMMUNITY EXCHANGE)

Na Mathias Canal, Dodoma
Serikali inaendelea na mchakato wa kufanikisha uwepo wa Mfumo wa soko la bidhaa (Commodity Exchange) ambapo miongoni mwa kazi za Mfumo huo utalenga kupunguza gharama za uendeshaji wa masoko ya mazao yote ya chakula na biashara ili kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri na yenye tija.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa Bungeni Mjini Dodoma Wakati akijibu swali la Mbunge wa Lulindi Mkoani  Mtwara Mhe JEROME DISMAS BWANAUSI aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanzisha mfumo wa “Commodity Exchange” ili kuwasaidia wananchi wanaolima Korosho kupata bei nzuri katika misimu husika.
Mhe Naibu Waziri alisema kuwa Maandalizi ya Soko la Bidhaa (Commodity Exchange) yalianza tangu mwaka 2011 kwa lengo la kufanya biashara ya mazao kuwa ya wazi na yenye ushindani kulingana na nguvu ya soko.
Mhe Mwanjelwa alizitaja hatua ambazo zimechukuliwa na serikali mpaka hivi sasa kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa Waraka wa Soko hilo, Kuundwa kwa Bodi ya Soko, kutungwa kwa Sheria ya mwaka 2015 ya Soko la Bidhaa pamoja na kanuni zake, Kufanya uzinduzi wa kuanzisha Soko hilo, Kutoa mafunzo kwa Madalali watakaoendesha soko hilo na Kutoa mafunzo kwa baadhi ya viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi ili kujenga uelewa wa pamoja.
Alisema, Ofisi na Jukwaa la soko hilo vimefunguliwa katika jengo la LAPF lililoko Kijitonyama jijini Dar es Salaam ambapo kazi za uwekaji wa vifaa katika Ofisi na Jukwaa hilo zinaendelea. 
Mhe Mwanjelwa alisema, Elimu ya Soko la Bidhaa inaendelea kutolewa kwa baadhi ya viongozi wa ngazi za Mkoa na Wilaya na Maafisa Kilimo, Ushirika, Biashara na Maendeleo ya Jamii katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro, Dodoma na Singida.
Aidha, elimu hiyo imekwisha kutolewa kwa Viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Viongozi wa Vyama vya Msingi na Vyama visivyokuwa vya Kiserikali ili kujenga uelewa wa soko hilo. Pia, elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima na wananchi kwa ujumla ili wadau waufahamu mfumo huo wa soko.
Kuhusu suala la kodi kwa wakulima wa korosho Mhe Naibu Waziri alisema kuwa Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeondoa ushuru na tozo na kubakiza makato ya usafirishaji korosho kulingana na umbali halisi, mchango wa kuendeleza zao na ushirika na kuondoa shilingi 50 kwa kila kilo zilizokuwa zinatozwa kwa ajili ya kufungashia korosho. Aidha, Serikali imepunguza ushuru kwa Halmashauri za Wilaya kutoka asilimia 5 hadi 3.
Sambamba na hayo pia Naibu Waziri Mhe Mwanjelwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Busokelo Mhe Fredy Atupele Mwakibete Mkoani Mbeya kuhusu ujenzi wa chuo cha kilimo na mifugo Kata ya Lufilyo alisema kuwa Wizara ya Kilimo ina jukumu la kusimamia na kuviendeleza Vyuo vya Kilimo hapa nchini. 

Alisema, Kwa mujibu wa maelezo ya Afisa Kilimo wa Wilaya ya Busokelo, Chuo kilichotajwa na Mhe. Mbunge sio Chuo cha Kilimo na Mifugo bali ni Kituo kidogo cha kutoa mafunzo ya kilimo kwenye Skimu za Umwagiliaji (Ward Agricultural Resource Centre).  Kituo hicho kilijengwa kwa jitihada za aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki Mheshimiwa Profesa Mark Mwandosya ambapo mwisho alikabidhi kituo hicho kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ili wakamilishe sehemu iliyobaki.

Aliongeza kuwa Wizara inatambua uwepo wa kituo hicho na inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ili kupata fedha za kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa ajili ya kutumika kama ilivyokusudiwa.

Vyuo vya Kilimo vinavyosimamiwa na Wizara ya Kilimo viko 14.  Vyote hivyo vimejengwa muda mrefu na hivi sasa vinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ikiwemo Ofisi za Walimu, Madarasa, Mabweni, Maabara, Nyumba za walimu, Maktaba na Karakana.  Changamoto zingine ni uhaba wa Wakufunzi na Watumishi wa kada zingine pamoja na vifaa vya kufundishia.

Aidha, Kutokana na changamoto hizo Wizara imeweka kipaumbele cha kuboresha Vyuo vilivyopo badala ya kufikiria kuongeza Vyuo vingine. 

Mhe Mwanjelwa alisisitiza kuwa Vyuo hivyo vikiakarabatiwa vitaweza kuchukua wanafunzi wengi hivyo kuwezesha Serikali kufikia lengo la kuwa na mtaalamu mmoja wa kilimo katika kila kijiji na pia kuzalisha Maafisa Ugani wenye uwezo wa kutoa huduma bora kwa wakulima. 

Aidha, katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 Serikali imeshatenga shilingi 773,208,000/= kwa kuanzia kwa ajili ya kufanya ukarabati katika Vyuo vya MATI.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com