Na
Mathias Canal, Dodoma
Serikali inaendelea na
mchakato wa kufanikisha uwepo wa Mfumo wa soko la bidhaa (Commodity Exchange) ambapo
miongoni mwa kazi za Mfumo huo utalenga kupunguza gharama za uendeshaji wa
masoko ya mazao yote ya chakula na biashara ili kuwawezesha wakulima kupata bei
nzuri na yenye tija.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa Bungeni Mjini Dodoma Wakati
akijibu swali la Mbunge wa Lulindi Mkoani Mtwara Mhe JEROME DISMAS BWANAUSI aliyetaka
kufahamu ni lini Serikali itaanzisha mfumo wa “Commodity Exchange” ili kuwasaidia wananchi wanaolima Korosho
kupata bei nzuri katika misimu husika.
Mhe Naibu Waziri alisema
kuwa Maandalizi ya Soko la Bidhaa (Commodity
Exchange) yalianza tangu mwaka 2011 kwa lengo la kufanya biashara ya mazao
kuwa ya wazi na yenye ushindani kulingana na nguvu ya soko.
Mhe Mwanjelwa alizitaja hatua ambazo zimechukuliwa na serikali
mpaka hivi sasa kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa Waraka wa Soko hilo, Kuundwa
kwa Bodi ya Soko, kutungwa kwa Sheria ya mwaka 2015 ya Soko la Bidhaa pamoja na
kanuni zake, Kufanya uzinduzi wa kuanzisha Soko hilo, Kutoa mafunzo kwa
Madalali watakaoendesha soko hilo na Kutoa mafunzo kwa baadhi ya viongozi wa
Serikali na Sekta Binafsi ili kujenga uelewa wa pamoja.
Alisema, Ofisi na Jukwaa
la soko hilo vimefunguliwa katika jengo la LAPF lililoko Kijitonyama jijini Dar
es Salaam ambapo kazi za uwekaji wa vifaa katika Ofisi na Jukwaa hilo
zinaendelea.
Mhe Mwanjelwa alisema, Elimu ya Soko la Bidhaa inaendelea
kutolewa kwa baadhi ya viongozi wa ngazi za Mkoa na Wilaya na Maafisa Kilimo,
Ushirika, Biashara na Maendeleo ya Jamii katika mikoa ya Lindi, Mtwara,
Morogoro, Dodoma na Singida.
Aidha, elimu hiyo
imekwisha kutolewa kwa Viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Viongozi wa
Vyama vya Msingi na Vyama visivyokuwa vya Kiserikali ili kujenga uelewa wa soko
hilo. Pia, elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima na wananchi kwa ujumla ili
wadau waufahamu mfumo huo wa soko.
Kuhusu suala la kodi kwa
wakulima wa korosho Mhe Naibu Waziri alisema kuwa Katika mwaka wa fedha
2017/2018, Serikali imeondoa ushuru na tozo na kubakiza makato ya usafirishaji
korosho kulingana na umbali halisi, mchango wa kuendeleza zao na ushirika na
kuondoa shilingi 50 kwa kila kilo zilizokuwa zinatozwa kwa ajili ya kufungashia
korosho. Aidha, Serikali imepunguza ushuru kwa Halmashauri za Wilaya kutoka
asilimia 5 hadi 3.
Sambamba na
hayo pia Naibu Waziri Mhe Mwanjelwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la
Busokelo Mhe Fredy Atupele Mwakibete Mkoani Mbeya kuhusu ujenzi wa chuo cha
kilimo na mifugo Kata ya Lufilyo alisema kuwa Wizara ya Kilimo ina jukumu la
kusimamia na kuviendeleza Vyuo vya Kilimo hapa nchini.
Alisema, Kwa
mujibu wa maelezo ya Afisa Kilimo wa Wilaya ya Busokelo, Chuo kilichotajwa na
Mhe. Mbunge sio Chuo cha Kilimo na Mifugo bali ni Kituo kidogo cha kutoa
mafunzo ya kilimo kwenye Skimu za Umwagiliaji (Ward Agricultural Resource Centre).
Kituo hicho kilijengwa kwa jitihada za aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la
Rungwe Mashariki Mheshimiwa Profesa Mark Mwandosya ambapo mwisho alikabidhi
kituo hicho kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ili wakamilishe sehemu
iliyobaki.
Aliongeza
kuwa Wizara inatambua uwepo wa kituo hicho na inaendelea kushirikiana na wadau
mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ili kupata fedha za
kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa ajili ya kutumika kama ilivyokusudiwa.
Vyuo
vya Kilimo vinavyosimamiwa na Wizara ya Kilimo viko 14. Vyote hivyo vimejengwa muda mrefu na hivi sasa
vinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu
ikiwemo Ofisi za Walimu, Madarasa, Mabweni, Maabara, Nyumba za walimu, Maktaba
na Karakana. Changamoto zingine ni uhaba
wa Wakufunzi na Watumishi wa kada zingine pamoja na vifaa vya kufundishia.
Aidha, Kutokana na changamoto hizo Wizara
imeweka kipaumbele cha kuboresha Vyuo vilivyopo badala ya kufikiria kuongeza
Vyuo vingine.
Mhe
Mwanjelwa alisisitiza kuwa Vyuo hivyo vikiakarabatiwa vitaweza kuchukua
wanafunzi wengi hivyo kuwezesha Serikali kufikia lengo la kuwa na mtaalamu
mmoja wa kilimo katika kila kijiji na pia kuzalisha Maafisa Ugani wenye uwezo
wa kutoa huduma bora kwa wakulima.
Aidha,
katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 Serikali imeshatenga shilingi
773,208,000/= kwa kuanzia kwa ajili ya kufanya ukarabati katika Vyuo vya MATI.
MWISHO
No comments:
Post a Comment