SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (Tanapa) litatumia
siku mbili za maonesho ya utalii ya Karibu Kusini yanayofanyika kwa wiki moja
mjini Iringa kutoa usafiri wa gharama nafuu kwa watu wanaotaka kutimiza ndoto zao
za kufanya utalii katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa.
Akizungumza na wanahabari jana, meneja masoko
wa shirika hilo, Victor Ketansi alisema kwa kupitia maonesho hayo
yatakayofanyika kati ya Septemba 27 na Oktoba 2, mwaka huu, Tanapa itafanya
safari hizo Septemba 28 na 30.
“Kwa kupitia ofa hiyo kutakuwa na mchango
mdogo wa fedha; mtu mzima atalazimika kuchangia Sh 30,000 na mtoto Sh 10,000 tu
kumuwezesha kwenda kwa siku moja kutalii katika hifadhi hiyo kubwa kuliko zote
nchini,” alisema.
Alisema mchango huo unahusisha gharama ya
usafiri, kiingilio cha hifadhini, utalii na muongoza wageni atakayewapitisha
katika vivutio mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo.
“Tuna nafasi 50 tu tumetoa kwa kupitia
ofa hii. Safari ya kwanza itahusisha watu 25 na safari ya pili watu 25 pia,
kwahiyo wanaotaka wafike na kujiandikisha katika banda letu lililopo katika
viwanja vya Kichangani yanapofanyika maonesho haya,” alisema.
Akizungumzia baadhi ya vivutio vilivyoko
katika hifadhi hiyo, Mhifadhi wa Idara ya Utalii Ruaha, Hellen Mchaki alisema
Hifadhi ya Ruaha pamoja na wingi wa vivutio inabeba pia historia muhimu ya
Chifu Mkwawa, kiongozi wa kabila la Wahehe mkoani Iringa aliyeongoza mapambano
dhidi ya wajerumani katika karne ya 19.
Alitaja baadhi ya wanyama waliopo katika
hifadhi hiyo kuwa ni kudu wakubwa na wadogo, viboko, mamba, pofu, swala pala, makundi
makubwa ya samba, tembo na nyati, chui, mbweha, fisi, twiga, pundamilia na mbwa
mwitu.
Akizungumzia idadi ya watalii katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Mchaki alisema mwaka 2012/2013 walipokea
watalii wa nje 14,299 na wa ndani 9,094, mwaka 2013/2014 wa nje 13,489 na wa
ndani 9,673 na mwaka 2014/2015 wa nje 13,272 na wa ndani 8,291.
0 comments:
Post a Comment