Maonesho hayo yameandaliwa na mikoa ya
nyanda za juu kusini kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii,
shirika la kuhudumia viwanda vidogo (Sido) na wadau mbalimbali ukiwemo Mradi wa
Kuboresha Mtandao wa Maneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST).
Akizungumza na wanahabari jana, Mratibu
wa Spanest, Godwell Ole Meing’ataki alisema ushiriki wa wadau hao ni mafanikio
makubwa katika sekta ya utalii inayoanza kutumiwa na wajasiriamali hao kutangaza
bidhaa zao.
“Watu wa kusini wana fursa kubwa sana ya
kuongeza mapato yao kwa kupitia sekta hii ya utalii. Mikoa ya kusini ina
rasilimali na vivutio vingi, vikihifadhiwa na kulindwa vitaleta wageni wengi na
hivyo kuchochea shughuli zingine za maendeleo,” alisema.
Meing’ataki alisema maonesho ya mwaka huu
yamekuwa bora zaidi kwasababu kamati inayoyaratibu imejitahidi kwa kiwango
kikubwa kushughulikia changamoto mbalimbali zilizojitokeza mwaka jana wakati
yakifanyika kwa mara ya kwanza.
“Kwa Spanest haya ni mafanikio makubwa na
ni matokeo ya mradi wetu kusaidia kuwaleta wadau mbalimbali wa uhifadhi na
utalii ili waweze kwa pamoja kushughulikia changamoto mbalimbali katika maeneo
hayo,” alisema.
Katika uhifadhi, Meing’ataki alisema
SPANEST inayofadhiliwa na Shirika
la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF)
imefanya mengi yakiwemo mafunzo kwa askari wanyamapori na imetoa vifaa
mbalimbali vinavyosaidia kuboresha na kukabiliana na ujangili ndani na nje ya
maeneo yaliyohifadhiwa.
“Na kwa upande wa utalii tumekuwa tukiwapeleka wadau katika maonesho ya
Karibu Fair ya Arusha ili kujifunza na kutumia fursa hiyo kutangaza utalii na
shughuli za ujasiriamali zinazofanywa kusini,” alisema.
Katika kuboresha huduma za hoteli, alisema Spanest imetoa mafunzo kwa
watoa huduma na imeshiriki pia kuandaa mipango mikakati ya kuendeleza utalii katika
mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya.
Meing’ataki alisema maonesho ya utalii ya
Karibu Kusini yanaweza kuwa maonesho ya utalii ya kimataifa kwa kadri yanavyozidi
kukua na kwa kuzingatia fursa za kiuchumi na utalii zilizoko katika mikoa hiyo.
Alisema kukua kwa sekta hiyo ya utalii kunapaswa
pia kwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege,
mfumo mzima wa mawasiliano na vituo vya kutolea taarifa na kuhakikisha huduma za
hoteli na waongoza watalii zinaimarishwa ili kukidhi viwango vinavyotakiwa.
“Tunataka kuona miaka kadhaa ijayo
maonesho haya na vivutio vya utalii katika mikoa ya kusini vinaleta wageni wengi
zaidi na hilo likifanikiwa litasaidia kunyanyua shughuli za wajasiriamali na
mapato ya wakazi wa mikoa hiyo na hivyo kuhifurahi sekta hiyo,” alisema.
0 comments:
Post a Comment