METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, September 7, 2017

SERIKALI KURAHISISHA MAISHA YA WASTAAFU

PIX-4-6
Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mifumo ya kukusanya mapato pamoja na kuboresha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kuleta unafuu wa maisha ya Wastaafu na Wananchi kwa ujumla.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mtambile Mhe. Masoud Abdallah Salim (CUF), aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kuboresha mafao ya uzeeni ili kuondoa malalamiko ya hali ngumu ya maisha wanayoishi Wastaafu.

Mhe. Salim alisema kuwa kumekuwepo malalamiko mengi kutoka kwa Wastaafu ambao wakati wa utumishi wao walilitumikia Taifa kwa uwaminifu na uadilifu mkubwa, kuhusu kuishi maisha magumu yanayotokana na kucheleweshewa mafao yao ya uzeeni yasiyolingana na kupanda kwa gharama za maisha.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali kwa sasa imejielekeza zaidi katika kuboresha miundombinu ya  usafiri na usafirishaji, nishati ya umeme, maji, huduma za afya, elimu na kiuchumi hususan katika ukusanyaji mapato kwa lengo la kuboresha maisha ya Wastaafu na Wananchi kwa ujumla.

“Tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika juhudi zake za kujenga uchumi imara, uchumi wa viwanda ambao ndio msingi mkuu wa kuimarisha mapato ya Serikali”. Alisema Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa maboresho ya viwango vya pensheni kwa Wastaafu yasiyoendana na maboresho ya miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii hayawezi kuondoa malalamiko ya Wastaafu hivyo Serikali imelenga zaidi kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii ili kupunguza malalamiko hayo.

Dkt. Kijaji alifafanua kuwa nyongeza ya pensheni kwa Wastaafu, mishahara na maslahi mazuri kwa Watumishi wa Umma itaongezeka kama mikakati na azma ya Serikali ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi itafanikishwa.

Aidha Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni ili kukidhi mahitaji muhimu ya Wastaafu, kwa kutambua hilo Mwezi Julai 2015, Serikali iliboresha kiwango cha pensheni kutoka Sh. 50,114 hadi Sh. 100,125 kwa mwezi.

Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com