Rais
wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
(kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo
la Umoja wa Mataifa (FAO) Dkt.Jose Graziano da Silva alipofika Ikulu
Mjini Unguja leo,
Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na mgeni
wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa
(FAO) Dkt.Jose Graziano da Silva alipofika Ikulu Mjini Unguja
leo,[Picha na Ikulu.] 07/09/2017.
………………………..
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Shirika la
Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo
Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dk. Jose
Graziano da Silva, ambaye amefika Zanzibar kwa lengo la kuongeza
mashirikiano baina ya Shirika hilo na Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk.
Shein alimueleza Mkurugenzi Mkuu huyo kuwa FAO ni miongoni mwa Mashirika
ya Umoja wa Mataifa yalio na historia kubwa katika kuisaidia Zanzibar
katika sekta ya kilimo pamoja na mazao yanayohusiana na chakula.
Aliongeza kuwa FAO imeweza
kutoa misaada mbali mbali ya kuendeleza sekta ya kilimo hapa Zanzibar na
kumueleza Mkurugenzi Mkuu huyo jitihada za wananchi wa Zanzibar katika
kuliendeleza zao la mwani na kusisitiza haja kwa Shirika hilo kuiunga
mkono Zanzibar katika kuhakikisha kilimo hicho kinawanufaisha wakulima
wake.
Pamoja na hayo, Dk. Shein
alitoa pongezi za pekee kwa Shirika hilo kwa ushirikiano wake mkubwa
unaotoa katika kupambana na athari za kilimo zinazosababishwa na wadudu
waharibifu wa matunda ikiwa ni pamoja na utafiti wa maradhi ya zao la
mwani.
Aidha, Dk. Shein alimueleza
Mkurugenzi Mkuu huyo juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya kilimo na uvuvi pamoja na azma ya kuanzisha viwanda
vidogo vidogo ambavyo malighafi zake zitatokana na rasiliamali za sekta
hizo ili kwa pamoja ziweze kuwa na mchango mkubwa katika soko la ajira
hasa kwa vijana.
Dk. Shein alimueleza
Mkurugenzi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Wizara yake ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi katika
kuendeleza na kuimarisha sekta ya kilimo, uvuvi na uvugaji ili sekta
hizo ziweze kuleta tija na kutoa ajira hasa ikizingatiwa kuwa asilimia
70 ya wananchi wa Zanzibar wanajihusisha katika sekta hizo.
Hivyo, alimshauri Mkurugenzi
Mkuu huyo kuwa katika ziara yake ijayo ni vyema akatembelea kisiwani
Pemba kwa lengo la kuangalia juhudi za wananchi wa kisiwa hicho katika
kuendeleza sekta ya uvuvi na ufugaji hasa ufugaji wa samaki.
Sambamba na hayo, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika hilo la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Kilimo na Chakula Duniani pamoja na kumpongeza
Mkurugenzi Mkuu wake Dk. Graziano da Silva kwa kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar na kusaidia katika kuhakikisha sekta ya kilimo inazidi
kuimarika.
Nae Dk. Graziano da Silva
alimuhakikishia Dk. Shein pamoja na kuihakikishia Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono na kuisaidia
Zanzibar katika kuimarisha sekta ya Kilimo na kulipokea wazo la Rais Dk.
Shein la kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo wataalamu wa kituo cha
utafiti wa kilimo kilichopo Kizimbani.
Mkurugenzi Mkuu huyo alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa
uongozi wa Wizara husika ya Kilimo pamoja na ziara aliyofanya katika
maeneo mbali mbali yakiwemo mashamba ya viungo na maeneo ya utafiti
Kizimbani.
Hivyo, alieleza kuwa baada ya
ziara yake hiyo ameweza kugundua utajiri mkubwa ulionao Zanzibar wa
mazao ya viungo ambayo Shirika lake la FAO litaangalia namna ya kusaidia
ili bidhaa hizo za viungo ziweze kutengenezewa dawa za tiba asilia.
Dk. Graziano da Silva alisema
kuwa umefika wakati wa kuelekeza nguvu zote katika mageuzi ya kilimo
hatua ambayo itaimarisha zaidi uzalishaji wa mazao ambayo yataimarisha
sekta ya biashara sambamba na sekta ya viwanda hapa nchini.
Dk. Graziano da Silva alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa Zanzibar kwa kuendeleza ushirikiano na
uhusiano mwema uliopelekea mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo hapa
nchini kwa kuimarisha uhakika wa chakula na maendeleo ya ya sekta hiyo.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi
Mkuu huyo wa FAO aliipongeza Zanzibar kwa kuendeleza na kusimamia vyema
miradi yote inayoendeshwa na Shirika hilo na kusisitiza kuwa
limefarajika na juhudi hizo na itaendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo,
alimueleza Dk. Shein juhudi zinazochukuliwa na Shirika hilo la FAO
katika kuhakikisha usalama wa chakula unakuwa ni ajenda muhimu kwa nchi
za bara la Afrika kwani ni jukumu moja wapo la Shirika hilo.
0 comments:
Post a Comment