METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 27, 2020

BENKI YA TPB YATOA MSAADA WA TANI 10 ZA SARUJI KWA HOSPITALI YA BUGANDO MWANZA


Benki ya TPB Tanzania imetoa msaada wa tani 10 za mifuko ya saruji kwa hospitali ya Bugando Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa saratani wanaofika kupata huduma katika hospitali hiyo.

Msaada huo umekabidhiwa  March 26, 2020 kwa uongozi wa hospitali hiyo na Mkurugenzi Mkuu wa TPB-PLC Sabasaba Moshingi akiwa ameambatana na Meneja uhusiano wa TPB Chichi Banda, Mameneja wa TPB Benki matawi ya Mwanza Yoram Gwakisa(Kenyata), Alex Minai(Pamba) na Helen Kidayi(Liberty)

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo,  Mkurugenzi Mkuu wa TPB alisema msaada huo ni kuonyesha kuthamini wadau wanaowazunguka na wamekuwa na utaratibu wa kutenga fedha kila mwaka katika kuhudumia jamii.

"Benki yetu inathamini kushirikiana na wadau mbalimbali wanaotuzunguka na kila mwaka uwa tunatenga pesa kwa ajili ya kuhudumia jamii hasa katika masuala ya afya, elimu na huduma nyinginezo" alisema Mkurugenzi

Aidha ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kuanzisha huduma ya saratani katika Mkoa wa Mwanza ambapo awali wananchi kutoka mikoa ya Kanza ya Ziwa na kanda ya Magharibi walikuwa wakifuata huduma hiyo Jijini Dar es salaam.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya hospitali, Mkurugenzi wa Bugando Medical Centre Prof. Dkt Abel Makubi ameushukuru uongozi wa Benki hiyo akiamini kwamba wawekezaji ambao ni watanzania wataona thamani ya uwekezaji wao kupitia bank hiyo.

"Tunaamini Watanzania ambao haswa ndiyo wawekezaji katika benki hii, wataona uwekezaji wao kwenye benki hii unazaa matunda na kurudi kwao katika kuwapa huduma kupitia misaada mbalimbali mnayoitoa" alisema Dkt Abel 

Dkt. Bingwa wa Saratani katika hyospitali hiyo Lucas Faustine Kiyegi alisema kukamilika kwa majengo hayo kutawapunguzia adha wagonjwa wanaopata huduma katika hospitali hiyo hususani wale wanaotoka mbali waliokuwa wanatakiwa kuwepo hospitalini kwa muda mrefu Zaidi.

"Hospitali hii inatoa huduma katika mikoa nane(8) na huduma za mionzi wakati mwingine mgonjwa analazimika kuwepo hospitalini kwa muda mrefu awali hakukuwa na mahali pa kuwalaza kwa hiyo kukamilika kwa majengo haya kutawaondolea usumbufu waliokuwa wakiupata" alisema Dkt Lucas

Msaada uliotolewa na Benki hiyo ni tani 10 za saruji yenye thamani ya shilingi 3,600,000.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com