Jiwe la msingi lililowekwa na Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani ikiwa ni kuzindua na kuwasha taa zinazotumia
mwanga wa jua( Solar) katika mitaa ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
Muonekano wa Kituo kipya cha Afya cha Bwina
nyakati za usiku baada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kuwasha umeme
katika kituo hicho.
Muonekano wa barabara za Mitaa za Chato
baada nyakati za usiku baada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani
kuzindua na kuwasha taa zinazotumia mwanga wa Jua(Solar).
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani
amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini,
kujikinga na kuchukuwa tahadhari dhidi ya virusi vya Corona ili kuendelea
kutekeleza miradi hiyo na kuikamilisha kwa wakati unaotakiwa kwa mujibu wa
mikataba.
Dkt. Kalemani alisema hayo, Machi 26, 2020,
wakati wa akiwasha umeme katika Kituo cha Afya cha Bwina,kuwasha taa za
barabarani zinazotumia mwanga wa jua( Solar)na kuwahamasisha wananchi kuendelea
kuchukuwa tahadhari na kujikinga dhidi ya virusi vya Corona katika Wilaya ya
Chato mkoani Geita.
Dkt. Kalemani alisema kuwa tishio dhidi
ya kuwepo kwa virusi vya Corona kusirudishe nyuma juhudi za utekelezaji wa
miradi ya usambazaji umeme vijijini kwa kuwa tayari mamlaka husika zimetoa
miongozo ya kujikinga na kujihadhari dhidi ya virusi hivyo katika maeneo
mbalimbali nchini.
“Tujikinge na tuchukue tahadhari dhidi
ya Corona, kazi ya kusambaza umeme vijijini lazima iendelee tena kwa kasi ya
hali ya juu na miradi ikamilishwe kwa wakati uliopangwa, cha muhimu ninyi
wakandarasi kufuata miongozo iliyotolewa na mamlaka husika ili muweze
kutekeleza majukumu yenu, lazima tufanye kazi tusambaze umeme, wananchi
wanataka umeme uwake,”alisema Dkt.Kalemani.
Alisema mamlaka husika zimeweka wazi na
kuendelea kutoa matangazo kila kona ya nchi hii ya namna bora ya kujikinga na
kuchukuwa tahadhari dhidi ya virusi vya Corona, hivyo wakandarasi katika maeneo
yao ya kazi kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza miongozo hiyo.
Akizindua na kuwasha taa za barabarani
katika mitaa ya Wilaya Chato mkoani Geita, Dkt.Kalemani alisema kuwa lengo la
kuweka taa hizo ni kuongeza usalama kwa wananchi wanaotumia barabara hizo
nyakati za usiku.
Aidha Dkt. Kalemani aliwasha umeme
katika Kituo kipya cha afya cha Bwina wilayani humo ili kurahisisha upatikanaji
wa huduma za afya wakati wote kwa wagonjwa wanaofika kutibiwa katika kituo
hicho.
Dkt. Kalemani aliwataka wananchi kulinda
miundombinu ya taa hizo pamoja na kuitunza ili idumu kwa muda mrefu kwa faida
yao na kuwahimiza wananchi kwenda kutibiwa wakati wote katika kituo cha afya
cha Bwina.
Katika ziara hiyo ,vilevile aliwasisitiza
wananchi kuendelea kutekeleza maagizo na maelekezo yanayoendelea kutolewa na
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na wadau mbalimbali wa
afya ya kujikinga dhidi ya Virusi vya Corona, ikiwemo kunawa mikono mara kwa
mara, kuepuka misongamano na mikusanyiko na kutoa taarifa pale tu wanapomuona
mtu mwenye dalili za ugonjwa huo kama zinavyoelezwa katika matangazo.
Dkt. Kalemani alikuwa akifanya ziara
yake hiyo pasipo kuwa na mikutano ya kuzungumza na wananchi, kusimama umbali
mrefu kati yake na baadhi ya watu alioambatana nao, vyombo vya habari na kunawa
mikono kila baada ya kufika eneo husika na kupaka kitakasa mikono( Sanitizer)
ili kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.
Ikumbukwe kuwa Machi 24, 2020, katika Mkutano
wa Baraza la Mawaziri, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa alielekeza kuwa sehemu kubwa
ya ziara ya Mawaziri katika kutekeleza majukumu yao, iwe ni kuwahamasisha
wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujinga dhidi ya virusi vya Corona, kwa
kufuata njia bora na sahihi zinazotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto.
0 comments:
Post a Comment