METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, June 30, 2017

Waziri Mkuu Apigilia Msumari Mwingine Zuio la Kusafirisha Mahindi Nje ya Nchi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema msimamo wa Serikali wa kuzuia usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi uko pale pale.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo  jana Alhamisi Juni 29, 2017 Bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri  Mkuu wakati akijibu swali la Ritha Kabati  (Viti Maalumu) aliyetaka ufafanuzi kuhusu zuio la kusafirisha mazao nje ya nchi kwa mikoa yenye chakula cha ziada.

“Tumedhibiti na kuzuia usafirishaji wa chakula hasa mahindi kwenda nje ya nchi ili kuliepusha Taifa kukumbwa na baa la njaa kutokana na baadhi ya mikoa kutopata mavuno ya kutosha,

“Kuna maeneo kama ya Sengerema na Geita mahindi yamekauka, hivyo bado tuna upungufu wa chakula. Na hata bei ya chakula ipo juu, hatuna namna nyingine zaidi ya kudhibiti utokaji wa chakula kwenda nje na nawasihi wananchi tushirikiane katika jambo hili,” alisema.

Waziri Mkuu alisema kama kuna ulazima wa kusafirisha chakula kwenda nje ya nchi wahusika wakaombe kibali kutoka Wizara ya Kilimo,  Mifugo na Uvuvi na kibali kiwe cha kusafirisha unga na si mahindi.
"Nimeeleza sisi tumedhibiti kutoa mahindi nje bila ya kibali na kama kuna umuhimu wa kuyapeleka mahindi nje basi yasagwe ndani ili upelekwe 'unga' maana ukisaga kuna faida zake, pumba tunazitumia kwa chakula cha mifugo lakini pia mashine zetu tunazo sisitiza viwanda zitapata kazi ya kusaga pamoja na kutoa ajira" alisisitizia Majaliwa. 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com