Wabunge
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliosimamishwa
kuhudhuria Bunge kwa mwaka mmoja, Ester Bulaya wa Bunda na Halima Mdee
wa Kawe, wamemfikisha mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai, wakipinga
kusimamishwa kwao.
Mwingine
ambaye wamemfikisha mahakamani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kinga, Haki
na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika, ambaye ni Mbunge wa Newala Mjini
(CCM).
Mbunge
wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliwaambia waandishi wa
habari jana kuwa tayari wabunge hao wamewasilisha shauri lao kwenye
Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma.
John
Mnyika ambaye alisimamishwa kuhudhuria vikao vya siku saba, adhabu
ambayo ilishaisha, naye ameungana na wabunge hao kwenye kesi hiyo.
"Leo
hii (jana) katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Mahakama Kuu
Dodoma waheshimiwa Ester Bulaya, Halima Mdee na John Mnyika wa Kibamba,
wamefungua maombi kuomba ruhusa ya mahakama wafungue mashtaka dhidi ya
Spika wa Bunge Job Ndugai, George Mkuchika na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, George Masaju," alisema Lissu.
Lissu
alisema waombaji wanaiomba mahakama kuu itoe amri ya kufuta uamuzi wa
Spika na wa Bunge kuwasimamisha John Mnyika kwa vikao saba na vile vile
ifute kabisa uamuzi wa Bunge wa kuwasimamisha kuhudhuria vikao
vilivyobaki na vikao vyote vya Mkutano wa nane na vikao vyote vya Bunge
la Tisa, Ester Bulaya na Halima Mdee.
Lissu
alisema adhabu zote hizo zinakwenda kinyume na sheria na zilitolewa na
Bunge hilo kama kuwakomoa wabunge hao watatu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni.
Hivi
karibuni, Spika Ndugai, aliwaonya wabunge hao kuwa wanaweza kukabiliwa
na adhabu kali zaidi ya ile waliyopewa endapo hawatachunga midomo yao.
Wabunge hao walisimamishwa Juni 5, mwaka huu, baada ya kutuhumiwa kudharau kiti cha Spika.
Mdee na Bulaya wamefungiwa kuhudhuria vikao vyote vilivyobaki vya Bunge hili na watakuwa nje mpaka Aprili mwakani.
Bulaya
na Mdee walisimamishwa baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Newala (CCM), George Mkuchika kutoa
taarifa ya makosa yao bungeni.
Azimio
hilo la Bunge lilifikiwa baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Juliana Shonza
(CCM) kutoa hoja ya kubadilisha azimio lililotolewa na Kamati ya Bunge
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
0 comments:
Post a Comment