Wednesday, June 21, 2017

Wapinzani Wampeleka Spika Ndugai Mahakamani

Wabunge  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliosimamishwa kuhudhuria Bunge kwa mwaka mmoja, Ester Bulaya wa Bunda na Halima Mdee wa Kawe, wamemfikisha mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai, wakipinga kusimamishwa kwao.

Mwingine ambaye wamemfikisha mahakamani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika, ambaye ni Mbunge wa Newala Mjini (CCM).

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tayari wabunge hao wamewasilisha shauri lao kwenye Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma.

John Mnyika ambaye alisimamishwa kuhudhuria vikao vya siku saba, adhabu ambayo ilishaisha, naye ameungana na wabunge hao kwenye kesi hiyo.

"Leo hii (jana) katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Mahakama Kuu Dodoma waheshimiwa Ester Bulaya, Halima Mdee na John Mnyika wa Kibamba, wamefungua maombi kuomba ruhusa ya mahakama wafungue mashtaka dhidi ya Spika wa Bunge Job Ndugai, George Mkuchika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju," alisema Lissu.

Lissu alisema waombaji wanaiomba mahakama kuu itoe amri ya kufuta uamuzi wa Spika na wa Bunge kuwasimamisha John Mnyika kwa vikao saba na vile vile ifute kabisa uamuzi wa Bunge wa kuwasimamisha kuhudhuria vikao vilivyobaki na vikao vyote vya Mkutano wa nane na vikao vyote vya Bunge la Tisa, Ester Bulaya na Halima Mdee.

Lissu alisema adhabu zote hizo zinakwenda kinyume na sheria na zilitolewa na Bunge hilo kama kuwakomoa wabunge hao watatu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Hivi karibuni, Spika Ndugai, aliwaonya wabunge hao kuwa wanaweza kukabiliwa na adhabu kali zaidi ya ile waliyopewa endapo hawatachunga midomo yao.
 
Wabunge hao walisimamishwa Juni 5, mwaka huu, baada ya kutuhumiwa kudharau kiti cha Spika.

Mdee na Bulaya wamefungiwa kuhudhuria vikao vyote vilivyobaki vya Bunge hili na watakuwa nje mpaka Aprili mwakani.

Bulaya na Mdee walisimamishwa baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Newala (CCM), George Mkuchika kutoa taarifa ya makosa yao bungeni.

Azimio hilo la Bunge lilifikiwa baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Juliana Shonza (CCM) kutoa hoja ya kubadilisha azimio lililotolewa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

No comments:

Post a Comment