Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imezindua jukwaa la uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake wa wilaya hiyo ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha inawainua kiuchumi sambamba na utekelezaji wa agizo la mlezi wa wilaya hiyo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu alilolitoa mapema mwaka huu
Uzinduzi wa Jukwaa hilo umejumuisha wanawake kutoka kata zote 19 za wilaya ya Ilemela na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo John Wanga Mkurugenzi wa Ilemela, Kheri James Katibu Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ilemela, Mratibu Uwezeshaji wananchi mkoa Mwanza Sikindene Yesaya, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo ngazi ya Mkoa Bi Anne Gongwe akiwa na Katibu wake Bi Grace Bunyinyiga na Wataalamu wa Manispaa Ilemela
Akizungumza wakati wa Uzinduzi huo mgeni rasmi na mkuu wa wilaya ya Ilemela Dkt Leonard Masale amewataka wanawake hao kulitumia jukwaa hilo katika kujadili fursa na changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi huku akiasa kutumika kama njia ya kujikwamua kiuchumi kwa kujihusha na shughuli za uzalishaji ili kuifikia Tanzania ya Viwanda
‘… Kajadilini fursa na mkazifahamu changamoto kisha mshiriki katika kuzipatia ufumbuzi kwa kufanya biashara au shughuli zozote za kiuchumi, Ndugu zangu Tunalo tatizo hatupeani taarifa na hizi fursa hatuwezi kuziona kama hatupeani taarifa …’ Alisisitiza
Kwa upende wake Mkurugenzi wa Ilemela John Wanga akimkaribisha Mgeni rasmi amemuhakikishia kuwa Manispaa yake kupitia baraza la madiwani itaendelea kutoa ushirikiano na kusaidia wanawake kuweza kujikwamua kiuchumi kama inavyofanya sasa kwa kutoa mapato yake ya ndani kwa kina mama na vijana waweze kujikwamua kiuchumi
Nae Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Kheri James amewahakikishia wanawake waliohudhuria uzinduzi huo kuwa Mbunge wao na naibu Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angeline Mabula pamoja na majukumu ya kitaifa aliyonayo anatambua changamoto wanazokumbana nazo na kuongeza kuwa ataendelea kuwasemea na kuwapigia katika kuhakikisha wanawake wanajikwamua kimaendeleo
Uzinduzi huo ulihitimishwa kwa zoezi la kuchagua viongozi wa jukwaa hilo ambapo ndugu Winfride Mgendi alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Ulowa Paulo kuwa katibu wa jukwaa hilo kwa wilaya ya Ilemela
" Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga "
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
18.05.2017
0 comments:
Post a Comment