SHERIA ya Fedha ya Mwaka 2016 iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru
kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu,
imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato lililoanza
kushuhudiwa kutoka kampuni za simu.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka
ya Mawasiliano (TCRA), iliambiwa kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa
Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka huu, mwezi uliopita serikali
imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato, yaliyotolewa na kampuni za simu.
Taarifa hiyo ilitolewa jana kwenye Kamati ya Kudumu ya Miundombinu,
imeonesha Kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa
fedha zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360 kwa mwezi, lakini baada
ya mabadiliko ya sheria, Julai pekee mwaka huu imelipa Sh bilioni 1.9.
Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin
Barongo aliiambia kamati hiyo kuwa kwa upande wa Kampuni ya Tigo,
walikuwa wanatoa wastani wa Sh milioni 250 kwa mwezi, lakini sasa
wametoa Sh bilioni 1.48.
Barongo ambaye ni Meneja Msaidizi, Kitengo cha Walipa Kodi Wakubwa
TRA alikuwa akizungumzia namna Mtambo Maalumu wa Kusimamia Mawasiliano
na Udhibiti wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS) unaosimamiwa na Mamlaka
ya Mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha ukusanyaji mapato.
“Pamoja na mabadiliko ya sheria yaliyoanza mwezi Julai mwaka huu,
kampuni za simu zilikuwa zikitoza transfer, lakini sheria ilikuwa
haigusi kwenye kutoa, Baada ya hiyo, tuligundua kuwa sasa kamisheni
nyingi zilipelekwa kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye
transfer zinapungua,” alisema Barongo.
Aliendelea kusema, “Kwa hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi
ambayo tunatoza kwenye kuweka na kutoa, yametusaidia.” Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso
alisisitiza kuwa wabunge wanategemea Wizara ya Miundombinu kupitia sekta
ya mawasiliano, ichangie mapato mengi kwa serikali.
Baada ya Bunge kupitisha mabadiliko ya sheria ya fedha yaliyopitisha
utozaji kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na simu za
mkononi, ulijitokeza mjadala ambao baadhi ya watu walidai ushuru huo
utaathiri wateja wa kampuni za simu na benki.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alifafanua kwamba
serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha au
vyote kwa kadri itakavyotozwa akisisitiza kwamba utalipwa na benki na
kampuni na si mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala
itakayofanyika.
Wakati huo huo akielezea Mtambo Maalumu wa Kusimamia Mawasiliano na
Udhibiti wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS), Barongo alisema pia
umesaidia kwa kiwango kikubwa katika mapato kutoka kampuni za simu.
Barongo alisema kabla ya mwaka 2013, mtambo ulipokuwa haujapatikana,
walishindwa kujua kiwango cha kodi kutoka kwenye kampuni za simu.
Aliwaambia wabunge kuwa awali kulikuwa na tatizo kubwa la kufahamu ni
kwa kiwango gani kampuni za simu zinazalisha ikizingatiwa kwamba, mfumo
wa sasa wa ulipaji kodi ni wa kujitathmini.
“Kwa hiyo tunasema huu mfumo unasaidia, unaonesha sasa ni namna gani
sasa wanaweza (kampuni za simu) kutambua kuwa wanafuatiliwa kwa nyuma,”
alisema.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema mtambo huo
wa TTMS una kazi nyingi ikiwemo kutambua mawasiliano ya udanganyifu
katika mitandao na namba za ulaghai zinazotumika kwenye mawasiliano ya
kimataifa kinyume cha sheria.
Akizungumzia hoja za baadhi ya wabunge waliotaka kufahamu ni kwa nini
kampuni za simu haziko kwenye walipa kodi wakubwa 10 wa mwanzo ,
Barongo alisema hivi sasa zinapangwa kulingana na sekta. Hata hivyo
alisema, itakapokuja kwenye sekta ya mawasiliano, anaamini angalau
kampuni tatu za simu zitaonekana kwenye nafasi ya juu.
Aliisifu kampuni mpya ya Halotel akisema inafanya vizuri. Kwa upande
wa TTCL, alisema bado haijatoa mchango wa kutosha katika mapato ya
serikali, jambo aliloshauri kuwa inahitaji kusaidiwa hatimaye iwe
miongoni mwa vyanzo vya mapato ya serikali.
Tuesday, August 30, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Na Mathias Canal, WEST-Rombo Ndizi ni zao kubwa la biashara na chakula hivyo likitumika vizuri litabadili uchumi wa wakulima na nchi kwa uju...
-
Kaimu mkurugenzi mkuu wa kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) Clifford Tandari Julia akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani alik...
-
" Asubuhi baada kusikia kilio cha Vijana wanaojituma wakilalamika kukosa mikopo toka Halmashauri hasa 5% za Vijana na wanawake" Sh...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment