NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR
SERIKALI ya Marekani imesema itaendelea
kutoa misaada ya Kiuchumi, Ustawi wa jamii na kisiasa kwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ili kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili.
Msimamo huo umeelezwa katika ziara ya
Ujumbe wa Serikali ya Marekani uliotembelea Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya sera za kiuchumi, kisiasa
na kijamii huko Afisi Kuu Kisiwandui Unguja.
Marekani ambayo ni miongoni mwa Taifa
kubwa lililoendelea kiuchumi, kijamii na kiulinzi hata katika masuala ya
Kisiasa limesema kasi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu
ya saba Zanzibar, linaishawishi taifa hilo kutoa misaada binafsi na
inayopitia katika ngazi za kimataifa, ili kuenzi kwa vitendo juhudi
hizo.
Hayo yameelezwa na Kiongozi wa Msafara
huo ambaye ni Afisa wa kusimamia Masuala ya sera za kijamii na kisisa
katika Ukanda wa Nchi za Afrika zilizomo katika jangwa la sahara, Bw.
Gregory Simpkims wakati Akizungumza na Viongozi na Maafisa wa CCM
waliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma
Abdallah “ Mabodi” hapo Kisiwandui Unguja.
Bw. Simpkims alieleza kwamba Chama cha
Mapinduzi (CCM) kimekomaa kisiasa na kinaendelea kuimarika tofauti na
vyama vya kisiasa vya nchi nyingine , barani Afrika ambavyo baadhi yao
vimeanza kupoteza nguvu na kuondolewa madarani na vyama vya upinzani.
“ Tuna nia ya kuisadia Zanzibar misaada
mbali mbali ili iweze kukuza uchumi wake katika masuala ya kiuchumi,
kijamii na kuimairisha mahusiano ya kibiashara.
Pia tunaamini kuwa vyama vya siasa
vilivyopo Zanzibar vitaendelea kulinda Amani ya Visiwa vya Zanzibar
bila kuruhusu ili viwe sehemu tulivu inayoshawishi kila taifa kufanya
utalii na shughuli nyingine za kijamii.
Akitoa ufafanuzi juu ya ugeni huo,
Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Abdallah Juma Abdallah “ Mabodi”
alifafanua kwamba ujumbe huo pamoja na masuala mengine umesifu suala la
serikali kuimarisha Amani na Utulivu wa nchi licha ya kuwepo kwa
changamoto za kisiasa visiwani humo.
Pia ujumbe huo ulitaka kujua njia na
sera zinazotumiwa na CCM kuendelea kuaminiwa na wananchi wa Tanzania na
Zanzibar kwa ujumla, hali inayopekea kuimarika kwa uchumi wa nchi hiyo.
Alisema kwamba ujumbe huo ulitaka kujua
mambo mbali mbali yakiwemo suala la Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka
2015, siri ya kuimarika kwa CCM kisiasa na utekelezaji wa
Mipango(Programs) ya maendeleo na ustawi wa kiuchumi wa Taifa la
Marekani na sera za nchi za nje za taifa hilo kwa upande wa Zanzibar.
Alisema walizungumzia uimarishaji wa
sera za kibiashara na kiuchumi ya Nchi za Afrika ambayo ni African
Growth and Opportunity Act (AGOA), Mpango huo una Sheria inayorahisisha
bidhaa kutoka Afrika ziingie katika soko la Marekani, na kueleza kuwa
kwa sasa wapo tayari Zanzibar kunufaika na Mkakati huo ili Bidhaa zake
zikauzwe katika soko hilo.
Dkt. Mabodi alisema ujumbe huo uliohoji
kwa nini Taarifa ya wasimamizi wa kimataifa wa Uchaguzi (International
Observers) wa mwaka 2015, ilikuwa tofauti na taarifa iliyotolewa na Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Alifafanua kwamba jawabu la swala hilo
Dkt. Mabodi alisema kwamba CCM inaamini na kuunga mkono taarifa na
maelekezo ya Tume hiyo kwani ndio iliyokuwa ikisimamia shughuli za
Uchaguzi toka awali na ilibainisha sababu kuu zaidi ya Tisa
zilizosababisha Uchaguzi huo kufutwa, na hao waangalizi wa uchaguzi wa
kimataifa walikuta mchakato huo ushaanza pia hawana uelewa wa kutoka juu
ya siasa za Zanzibar.
Hata hivyo alisema kwamba pamoja na
mambo mengine walitaka kujua kama ZEC wamewahi kutoa taarifa ya
tathimini ya uchaguzi huo, na kuelezwa kuwa tayari imetolewa na
kukabidhiwa rasmi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.
“ Wamezungumzia migogoro ya kisisa
iliyozunga Zanzibar toka kumalizika kwea Uchaguzi Mkuu wa Octobar 25,
2015 nami nikawambia mizozo kama hiyo kisisa hasa katika mifumo ya
kidemokrasia ni ya kawaida na kuwatolea mfano ambao hawakuupenda lakini
sikuewa na namna ikabidi niwaulize kuwa katika Nchi yao toka kumalizika
Uchaguzi Mkuu wa Rais Trump mbona mpaka leo, kuna shutuma na mizozo
mbali mbali ikiwemo kuilaumu Urusi kuwa iliingilia masuala ya uchaguzi
lakini pia Viongozi mbali mbali wamekuwa wakijiuzulu, na kuwahohoji ni
Taifa gani limeingilia mambo yao ya siasa za ndani hawakuwa na jawabu
rasmi la kunijibu”, alisema Dkt. Mabodi.
Sambamba na hayo Kiongozi huyo wa CCM
Zanzibar, aliweka wazi kuwa alichojifunza kupitia mazungumzo hayo ni
kuwa siasa na sera za kimataifa ni tofauti na Tanzania, kwani Nchi hizo
zinatambua uhalisia wa siasa za Zanzibar licha ya kuwepo na baadhi ya
wanasiasa wanaopotosha na kuchochea vurugu.
Alisema pamoja na hayo ujumbe huo wa
Ubalozi wa Marekani ulitaka Viongozi wa CCM kukaa meza moja na CUF
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa uliozuka toka kufutwa kwa
uchaguzi wa Octoba 2015, lakini Dkt. Mabodi akawafahamisha kwamba Chama
chake kimeshamaliza Uchaguzi na Tayari Rais wa Zanzibar Dkt. Shein
aliyepatikana kwa misingi ya kidemokrasia ataendelea kuongoza nchi hadi
Uchaguzi wa 2020.
Alisema kuwa tayari baada ya Uchaguzi
ulioharibika CCM kupitia viongozi wao waliitisha mazungumzo na CUF,
lakini kabla ya kufikia makubaliano Maalim Seif Sharif Hamad alisusia
mazungumzo hayo bila kutoa sababu za msingi.
Hata hivyo alisema Chama hicho kipo
tayari kukaa na CUF kujadili utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka
2015/2020 pamoja na sera mbali mbali za SMZ, lakini sio kwa suala la
Uchaguzi Mkuu uliopita.
Pia aliwambia wageni hao kuwa CCM
imekuwa ikijitahidi kuwambia wananchi walinde Amani na Utulivu wa nchi
na waendelee na shughuli za ujenzi wa Taifa kimaendeleo , lakini vyama
vya Upinzani navyo vimekuwa vikipandikiza mbegu za chuki kwa kuwambia
baadhi ya wananchi kwa maeneo tofauti wagome kushiriki katika harakati
hizo.
0 comments:
Post a Comment