Jumla ya wagonjwa 11 wamefanyiwa
upasuaji wa moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na
madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa ushirikiana na madaktari wenzao wa Taasisi ya Open
Heart International ya nchini Australia.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa
Upasuaji wa Moyo ambaye pia ni Daktari bingwa wa upasuaji wa Moyo Bashir
Nyangasa wakati akielezea jinsi kambi hiyo ya upasuaji inavyoendelea
kutoa matibabu kwa wagonjwa.
Dkt. Nyangasa alisema, “Kwa kushirikiana
na washirika wetu wa OHI tulianza kambi maalum ya upasuaji kuanzia
tarehe 10/03/2017 hadi leo tarehe 17/3/2017 tumefanya upasuaji kwa
wagonjwa 11 ambao wanaendelea vizuri, kati ya hao watoto ni tisa na
watu wazima ni wawili”,.
Dkt. Nyangasa alisema katika kambi hiyo
ambayo inamalizika tarehe 17/3/2017 walipanga kufanya upasuaji kwa
wagonjwa 25 kati ya hao watoto ni 15 na watu wazima ni 10.
Kuhusu uhitaji wa damu kwa wagonjwa
wanaofanyiwa upasuaji wa Moyo Dkt. Nyangasa alisema wagonjwa hao
wanahitaji damu nyingi hivyo basi aliwaomba wananchi wajitokeze
kuchangia damu ambayo itatumika kwa wagonjwa.
“Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi
kuchangia damu na uchangiaji huu wa damu usifanyike mara moja bali
uwe endelevu kwani Taasisi inatoa huduma kwa wagonjwa wakati wote siyo
wakati wa kambi maalum za matibabu ya moyo pekee yake”, alisisitiza
Dkt. Nyangasa.
Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2017 JKCI
kwa kushirikiana na baadhi ya washirika wake wa nje ya nchi ambao ni
Madaktari Afrika wa Marekani, Hospitali za Apolo Bangalore na BLK
zote za nchini India na Open Heart International ya Australia wamefanya
matibabu ya moyo ya kufungua na bila kufungua kifua kwa wagonjwa wa
moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia (OHI) wakifanya upasuaji wa kuziba matundu ya moyo kwa mgonjwa wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo inayoendelea katika Taasisi hiyo. Tangu kuanza kwa kambi hiyo tarehe 12/03/2017 hadi leo tarehe 14/03/2017 jumla ya wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji kati ya hao watoto ni tisa na watu wazima wawili.
Madaktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa
ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana
na wenzao wa Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia
(OHI) wakifanya upasuaji wa kuvuna mshipa wa damu mguuni kwa mgonjwa wa
moyo na kuupandikiza katika mishipa ya moyo iliyoziba kwa jina la
kitaalamu Coronary Artery Bypass Graft (CABG).
Tangu kuanza kwa kambi
hiyo tarehe 12/03/2017 hadi leo tarehe 14/03/2017 jumla ya wagonjwa 11
wamefanyiwa upasuaji kati ya hao watoto ni tisa na watu wazima wawili.
Habari/Picha na Anna Nkinda – JKCI.
0 comments:
Post a Comment