METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, June 27, 2020

RAIS DKT. MAGUFULI ATOA MAAGIZO KWA MKANDARASI

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale (kulia) na Mwakilishi wa Kampuni ya China  Railway 15 Bureau Group Corporation, Su Jinlan  wakionyesha nakala za mkataba wa makubaliano kati ya serikali na Kampuni hiyo ya ujenzi wa barabara ya Nanganga -Ruangwa yenye urefu wa Kilomita 53.2 kwa  gaharama ya Sh. Bilioni 59.28. Mkataba huo ulitiwa saini  huku ukishuhudiwa na Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa kwenye uwanja wa Likangala, Ruangwa Juni 27, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Elias Kuandikwa wakishuhudia wakati Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale na Mwakilishi wa Kampuni ya China  Railway 15 Bureau Group Corporation, Su Jinlan  wakitia saini mkataba wa makubaliano kati ya serikali na Kampuni hiyo ya ujenzi wa barabara ya Nanganga -Ruangwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 53.2 kwa gaharama ya Sh. Bilioni 59.28. Utiaji saini wa Mkataba huo ulifanyika kwenye uwanja wa Likangala , Ruangwa, Juni 27, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China aliyesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa km 53.2 kwa gharama ya sh. 59,286,553,159 aanze kazi mara moja.

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Juni 27, 2020) alipozungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwa njia ya simu alipompigia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa tukio la utiaji saini mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa barabara ya Ruangwa-Nanganga km 53.2 kwa kiwango cha lami.

“Nashukuru ahadi niliyoitoa leo imeanza kuzaa matunda na ilimradi mkandarasi amekubali kusaini aanze mara moja kupeleka mitambo kwenye eneo la mradi na nitakuja kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo.”

Pia, Rais Dkt. Magufuli ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi kwa uhodari wake katika kufanya kazi. “ Endeleeni kumuani Mheshimiwa Majaliwa, amekuwa akinisaidia. Aendelee kuchapa kazi kwa ajili ya Ruangwa na Tanzania.”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuthamini na kujali maendeleo ya Watanzania wakiwemo na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwa sababu ujenzi wa barabara ya Ruangwa hadi Nanganga kwa kiwango cha lami ni utekelezaji wa ahadi yake.

“Leo hii ni siku ya kihistoria kwa sababu kile ambacho tulikuwa tunatamani, kikaahidiwa hapa na kiongozi wa nchi Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya ziara Ruangwa aliweza kuvunja kiu yetu Wana-Ruangwa toka alivyokuwa anaingia Nanganga wananchi walimuomba asimame na yeye alisimama akijua kuwa hawa wana hamu ya maendeleo.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya Rais Dkt. Magufuli kusimama  aliwaambia kuwa “najua hamu yenu ni ya maendeleo, lakini mimi ninaanza kuwaondolea kiu ya muda mrefu ya barabara yenu kutoka hapa Nanganga mpaka Ruangwa kwa kuijenga kwa kiwango cha lami. Sifa moja ya Rais Dkt. Magufuli ni kusema na kutenda na ametekeleza.”

Vilevile, Waziri Mkuu amewataka Watanzania wote waendelee kushirikiana bila ya kujali itikadi zao za kisiasa kwa sababu maendeleo hayana chama na miradi ya maendeleo anayoitekeleza katika maeneo mbalimbali nchini imekuwa ikiwanufaisha wananchi wote.

Akizungumzia kuhusu Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China iliyosaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganaga kwa kiwango cha lami, Waziri Mkuu amesema ni miongoni mwa kampuni kubwa zinazojenga kwa viwango.

Waziri Mkuu ameendelea kuwashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa umoja na mshikamano mkubwa waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano na amewaahidi kuendelea kuwatumikia bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kwamba waendelee kuiunga mkono Serikali ambayo imefanikiwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 kwa vitendo.

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Ujenzi, Dkt. Elias Kuandikwa amesema barabara hiyo itakuwa na madaraja makubwa matatu na makaravati 31 na kwamba itajengwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyohitajika.

Dkt. Kuandikwa aliongeza kuwa barabara zingine za mkoa wa Lindi zikiwezo za kutoka Nachingwea hadi Liwale yenye urefu wa km 159 ipo katika hatua ya usanifu na barabara ya kutoka Liwale hadi Nangurukuru km 230 na Nanganga-Nachingwea-Masasi zipo katika utaratibu wa ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mapema, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale alisema barabara ya Nachingwea - Ruangwa - Nanganga ni barabara muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Lindi  kwani inaunganisha pia mkoa wa Lindi na mikoa jirani kwa barabara kuu ya Mtwara – Dar es Salaam na Mtwara – Masasi – Songea.


“Ili kurahisisha utekelezaji, mradi huu umegawanywa katika sehemu mbili: Sehemu ya Nachingwea hadi Ruangwa yenye urefu wa kilometa 52.8 na sehemu ya pili ni kutoka Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 53.2. Serikali imeamua kuanza ujenzi wa sehemu ya Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 53. 2 na upana wa meta 10.0, kwa kutumia fedha za ndani na itajengwa kwa muda wa miezi 27.”

Mhandisi Mfugale aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika utasaidia kukuza kilimo na utalii katika wilaya ya Ruangwa na mkoa wa Lindi kwa ujumla. Aidha mradi utakapokamilika utachochea ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi waishio maeneo ya Ruangwa, Nanganga na Nachingwea.

Wakizungumza kuhusu ujenzi wa barabara hiyo wananchi wa wilaya ya Ruangwa walimshukuru Rais Dkt. Magufuli pamoja na Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa kwa uamuzi wao wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani itasaidia katika ukuaji wa uchumi.

Miongoni mwa wananchi hao ni pamoja na dereva wa basi litokalo Ruangwa kwenda Masasi, Omar Njinji ambaye amesema kutengenezwa kwa barabara hiyo kutarahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo, pia nauli zitapungua na maendeleo ya wilaya nayo yataimarika.

Dereva mwingine Issa Lingonda wanaishukuru sana Serikali kwa uamuzi wake wa kujenga barabara hiyo kwa sababu ubovu wake unasababisha magari kuharibika mara kwa mara. “Tunamshukuru sana Rais pamoja na Mbunge wetu kwani tutapumzika kwenda gereji maana siku mbili tunafanyakazi siku mbili gereji. Ikiwekwa lami vyombo vyetu vya usafiri vitadumu na nauli zitapungua.”
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com