Mwenyekiti wa chama cha Wakulima
wa Alizeti Mkoa wa Singida Athumani Sima akisisitiza jambo katika kikao
cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.
Meneja wa Mradi wa Faida Mali
Mkoa wa Singida Christopher Mkondya akiandika maoni ya wakulima wa
alizeti wakati wa majadiliano katika kikao cha wadau wa kilimo cha
alizeti.
Baadhi ya wakulima wa alizeti
wakiandika baadhi ya maelekezo, mapendekezo na maoni yaliyotolewa katika
kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa
Faida Mali.
Mkulima wa alizeti Kutoka kata ya
Kinampundu Wilaya ya Mkalama Samwel Laida akifafanua jambo katika kikao
cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida
Mali.
Mkurugenzi wa Faida Mali Mkoa wa Singida Tom Silayo akiwaelezea wakulima wa alizeti mambo ambayo mradi huo utayatekeleza.
Afisa Kilimo Sekretarieti ya Mkoa
wa Singida Mashaka Mlangi na Afisa Maendeleo ya Jamii Patrick Kassango
wakichukua maoni ya wakulima walioudhuria kikao cha wadau wa kilimo cha
alizeti kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji.
Wakulima wa zao la alizeti Mkoani
Singida wamepata uhakika wa mbegu bora ya alizeti ambayo itawasaidia
kuzalisha kibiashara tofauti na hapo awali walipokuwa wakipata mbegu
zisiso na uhakika wa mavuno mazuri.
Mwenyekiti wa chama cha Wakulima
wa Alizeti Mkoa wa Singida Athumani Sima amesema hayo mapema leo katika
mkutano wa wadau wa kilimo cha alizeti ulioandaliwa na mradi wa Faida
Mali kupitia Shirika la AMDT ambalo limejikita katika kusaidia wakulima
wa zao hilo kupata mbegu bora.
Sima amesema hapo awali wakulima
walikuwa wakinunua mbegu kwa wauzaji ambao sio waaminifu na hivyo
kutovuna vizuri kutokana na mbegu hizo kuota vibaya na kutoa alizeti
kidogo.
Amesema mradi wa Faida Mali
umewahakikishia kuwasaidia upatikanaji wa mbegu bora na ya kisasa na
hivyo kukifanya kilimo cha alizeti kuwa kama biashara nyingine ambazo
zina faida kubwa.
“Hawa Faida Mali sisi tunawaamini
kwakuwa wamekuwa wakishirikiana na serikali hivyo watatusaidia katika
kupata mbegu bora, tulikuwa tunaumizwa na wauzaji wengine akikuuzia
mbegu inaota hapa, pale haioti matokeo yake unapata hasara” amesema na
kuongeza kuwa,
“Mkulima akipata Mbegu bora hiyo
ni hatua ya kwanza ya mafanikio, kwakweli baadhi yetu tulianza kukata
tamaa kwa kuona tunapata hasara tu, unalima alizeti miaka mingi huoni
faida kubwa kama ambavyo unatarajia, lakini mradi huu umetuonyesha njia
ya mafanikio, nawaomba wakulima wengine waweze kujiunga katika vikundi
ili waweze kufikiwa na mradi huu au miradi mingine”, amesisitiza.
Naye Mkulima wa alizeti Kutoka
kata ya Kinampundu Wilaya ya Mkalama Samwel Laida amesema utaratibu wa
kununua alizeti kwa magunia ya lumbesa badala ya vipimo vya mizani
unawapunja wakulima na kuwafanya warudi nyuma kiuchumi.
Laida amesema wanunuzi wa alizeti
wanapakia alizeti katika magunia na kushindilia ambapo kipimo hicho sio
sahihi na hakilengi kumwinua mkulima hivyo basi mradi wa Faida Mali
unapowasaidia kutafuta masoko uangalie na vipimo vinavyotumika katika
kununua zao hilo.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi
wa Faida Mali Mkoa wa Singida Christopher Mkondya amesema ili wakulima
wazalishe kibiashara watawasaidia kupata mbegu bora na ya kisasa, kupata
huduma mbalimbali za ugani, masoko na kuwaunganisha wakulima hao na
huduma za kifedha.
Mkondya amesema kwa kushirikia na
Autainsurance watawasaidia wakulima kupata elimu ya faida za bima na
hivyo watakata bima ya mazao yao ili wakipata majanga yoyote kama vile
moto, mafuriko, au mbegu kutoota wataweza kufidiwa na kuepuka hasara.
Ameongeza kuwa kupitia watoa
huduma wao ambao ni Ersoko wamejipanga kutoa elimu kwa wakulima hasa kwa
kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno ambapo mkulima atapata taariza zote za
kilimo cha alizeti kulingana na eneo alipo kwa kumuelekeza mbinu za
kulima kisasa, muda wa kupanda, aina ya mbolea na taarifa za masoko ya
mazao yake.
0 comments:
Post a Comment