Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Serikali imeazimia kuachana na biashara ya kuingiza nguo za mitumba kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka 2018.
Maazimio
hayo yamebainishwa na Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama katika
uzinduzi wa mafunzo ya uanagenzi ya ushonaji nguo katika kiwanda cha
Tanzania Tooku Garments Company, Ltd.
Mhe.
Jenista Mhagama amesema kuwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
wamekubaliana kwamba ifikapo mwaka 2018 soko la Afrika Mashariki
halitaingiza nguo za mitumba kutoka nje.
Ameongeza
kuwa kwa kutekeleza azimio hilo Serikali imeandaa mafunzo ya
kuhakikisha vijana wengi wanapata stadi za kushona nguo nchini ili
kuwawezesha kufanya kazi katika viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa kwa
ajili ya kutengeneza bidhaa zetu wenyewe na kuacha kutegemea bidhaa
kutoka nje.
“Tumejipanga
kutekeleza azimio hili na kwa kushirikiana na kiwanda hiki tunategemea
kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 2,000 kwa mwaka katika stadi za
kubuni mitindo, kukata, kushona na kumalizia nguo” alisema Mhe. Jenista.
Aidha
Waziri huyo amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwani mafunzo hayo
yatawasaidia kuendana na viwango vya soko la kimataifa na mahitaji ya
soko la nguo kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kubuni mitindo,
kukata na kushona nguo zenye ubora wa kimataifa.
“Imani
yangu kuwa wataalamu waliopo katika kiwanda hiki watawapa ujuzi wa
kutosha na wengine wataweza kupata ajira katika kiwanda hiki tumieni
fursa hii mliyoipata ni ya pekee kwani mmebahatika kuwa miongoni mwa
wanafunzi wa kwanza kupata mafunzo chini ya Programu ya Kukuza Ujuzi
Nchini.
Mhe
Jenista amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatawezesha vijana kupata ajira
katika Viwanda, kujiajiri na hata kutoa ajira kwa wengine hivyo vijana
watumie fursa hiyo kutengeneza mtaji na kujiunga katika vikundi
vitakavyowawezesha kufungua viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza nguo
na kuendelea kukuza ujuzi waliopata.
Pia
Waziri Jenista ametoa wito kwa viwanda vingine kushirikiana na Serikali
kukuza ujuzi kwa vijana kupitia mafunzo ya uanagenzi na kuwahakikisha
kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha Vijana kupata mafunzo ya aina hiyo.
“Napenda
niwahakikishie kuwa Serikali iko bega kwa bega nanyi, fungueni viwanda
vingi sehemu mbalimbali katika nchi yetu, sisi kama Serikali
tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha rasilimali watu ya kuendesha
viwanda hivi inapatikana”
Mbali
na hayo Serikali inayo mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha
kuwa Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na kuwa na uchumi wa kipato cha
kati ifikapo mwaka 2025.
Serikali
iliingia makubaliano na kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Co. Ltd
kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 2,000 kwa mwaka katika stadi za
kubuni mitindo, kukata, kushona na kumalizia nguo .Jumla ya vijana 1,089
waliomba nafasi ya kupata mafunzo hayo yatakayoendeshwa kwa awamu tatu
na kwa sasa jumla ya vijana 430 wanapata mafunzo hayo.
0 comments:
Post a Comment