Ili
kupata majibu ni uhuru unaanzia wapi, nadhani ni vema tukarejea tena kwa
hadithi ya kweli ya mtaalamu wa saikolojia na tabia za binadamu Viktor
Frankl.
Frankl
alikuzwa kifikra kwa kutegemea mafunzo ya katika somo la saikolojia toka
kwa nguli Sigmund Freud. Nadharia za Freud zimejengwa katika msingi ya
kuwa tabia ya mwanadamu inajengwa au kuchongwa na hali ya nje ya
mazingira yanayomzunguka kwa asilimia zaidi ya 70. Kwa tafsiri nyingine
haiba (personality) na tabia (character) ya mtu zitaathiriwa sana na
hali ya nje au mazingira yanayomzunguka.
Kwa
msingi wa nadharia hiyo, ukomo na mfumo wa maisha ya mtu huwa mara
nyingi huwa inafungwa kutokana na hali inayomzunguka na inakuwa ngumu
kujikomboa kutoka hapo na kuishi maisha nje ya mfumo uliokuzunguka.
Frankl
alikuwa daktari bingwa wa afya ya akili na raia Austria wenye asili ya
Kiyahudi alikuwa kafungwa gerezani huko Ujerumani nyakati za dikteta na
mfashisti Adolf Hitler. Akiwa gerezani alipitia maisha ya mateso na
msoto ambao hayakujali kabisa utu. Kupitia mateso hayo, baba yake, mama
yake na mkewe waliaga dunia kufuatia zoezi la kutumbukizwa katika tanuru
la moto wa gesi.
Ni dada yake tu na yeye ndiyo walipona. Frankl alipata mateso na kufikia wakati wa kutojua uwezekano wa kuiona kesho na maisha yake yake yatakuwaje. Kutokana na hayo mara kwa mara alikuwa na maswali mawili, je anaweza “kuokoka” na tanuru la gesi na ataishi chini ya mateso hayo mpaka lini?.
Siku moja
akiwa pekee na utupu katika chumba, akajiuliza swali, uhuru wa mtu ni
kitu gani hasa? Ni uhuru upi ambao askari magereza wa kinazi hawawezi
kumwondolea kabisa hata ikiwa gerezani katika maisha magumu?
Kumbuka, askari wale walikuwa wanadhibiti mazingira yake (they had control over his environment) na kumtendea chochote chenye kuleta maumivu katika mwili wake.
Pamoja na
changamoto hizo za mateso, Frankl alikuwa anafahamu kuwa, utambulisho
wake hauwezi kupotea. Alijiona kuwa na uhuru wa kufikiri chochote kile
mbali na mateso anayopata.
Yeye kama msomi aliamua kuanza kupiga picha mpya na kupata taswira tofauti katika akili yake.
Kati ya msoto na mateso, alianza kujiona siku moja atakuwa darasani anafundisha baada ya kutoka “segerea ya huko”.
Baada
kuifunza akili yake na mwendelezo wa nidhamu ya hali ya juu kwa jinsi
anavyotakiwa kufikiri tofauti, akili yake, mihemko (emotions), mwenendo
wake gerezani na namna ya kuhusiana na wanyapara ilibadilika.
Mara
tabia yake ikabadilika na kukawa na uhuru wa mazungumzo ya kati yake na
wanyapara wanaomtesa.
Kwa namna flani alianza kuwajengea uwezo wale
wanyapara wale ili wajitambue na kujua kusudi la maisha yao (he
empowered his captors to know the sense of lpurpose in their lives).
Frankl
alitumia dhana ya utajiri alionao mtu akitambua kusudi la yeye kuishi na
faida ya kutoa mchango wake kwa kuwasaidia wengine kuishi maisha ya
uhuru na furaha.
Kukatisha
hadithi hii ya kweli, baada ya miaka 3 Viktor Frankil alikuwa mtu huru
nje ya gereza na aliweza kuwa mmoja wa wasemaji wa kujengea watu uwezo
(motivational speakers). Amendika vitabu kadhaa na moja ya vitabu
alivyouza sana kinaitwa Man's Search for Meaning (mtu kutafuta maana ya
maisha)
Naomba
Watanzania tujifunze kutoka kwa Frankl. Kiuhalisia Tanzania inapitia
katika changamoto kubwa ya kimtazamo kwa sasa. Ukisoma magazeti,
ukisikiza mijadala ya redioni, vijiweni na kwenye mitandao ya kijamii,
unaweza kuvurungwa sana kwa namna ambavyo lawama na manung’uniko ni
makubwa kuliko habari zenye matumaini.
Najaribu
kujiuliza, mzee Nelson Mandela aliekaa gerezani miaka 27 katika chumba
kidogo, kitanda chake kikiwa ni sakafu, choo chake kikiwa ni ndoo,
akifanyishwa kazi ngumu ya kuponda kokoto. Mandela aliruhusiwa
kuetembelewa na mtu mmoja tu garezani kwa mwaka, na kuwa na mazungumzo
yasiyozidi dakika 30 tu.
Kimsingi,
Frankl na Mandela ilitakiwa “wavunjike” kiakili kutokana na msoto
walioupata kutoka gerezani mmoja akiwa chini ya wanazi na mwingine chini
ya makaburu. Msingi mkubwa wa selo za wafungwa kama Mandela na Frankl
ni ilikuwa kuwavuruga kiakili na ndiyo maana wafungwa wengi wakitoka
gerezani huwa wamekata tamaa. Baadhi huwa wanajihusisha tena na uhalifu
ili warejee gerezani.
Najaribu
kujiuliza, ni Watanzania wangapi wanatambua maana ya kuishi hatima
(sense of purpose towards destiny) bila kujali changamoto au ugumu wa
mazingira yanayomzunguka au habari hasi anayoisikia?
Saulos
Tarseus mwanafalsafa na msomi wa sheria kule mashariki ya kati wakati
mmoja akiwahusia wanafunzi wake kwa barua, aliwaambia “...badilikeni kwa
kufanya upya akili zenu...” (be transformed by renewal of your mind).
Akili ya mtu ni kitu cha msingi sana ili afike kule anakotaka kwenda
bila kujali anapitia ugumu gani katika wakati aliopo kwa sasa. Je,
Watanzania, kila mtu kwa nafsi yake, anajua anataka kwenda wapi ndani ya
miaka kadhaa?
Vikwanzo
unavyopitia ni vikali kama vifungo na mateso ya Frankl au Mandela?
Unafikiria na kujiona uko nje ya gereza na kuwa Rais wa nchi yako au
mkurungenzi wa taasisi au kampuni lako? Mandela alifikia ndoto yake ya
kuwa rais wan chi yake. Frankl aliweza tena kuwa mhadhiri. Mpaka lini
lawama zielekezwa kwa bosi, mazingira, wazazi au hali ya kisiasa ilivyo
kwa sasa?
Mtu moja alipata kusema “The same boiling water that softens the potato hardens the egg. It's about what you're made of, not the circumstances”
Maji yale yale yanayochemka ambayo kiazi kinalainika ndiyo hayahayo ambayo yanafanya yai liwe gumu. Inategemea nini kimekutengeneza na si mazingira au hali ya nje iliyokuzunguka.
Nawatakiwa Heri za Krismas na sherehe za kupokea mwaka 2017.
Fredrick Matuja
fmatuja@hotmail.com
0 comments:
Post a Comment