Mkutano
kati ya Marekani, Urusi na nchi nyingine saba za kikanda, umeshindwa
kufikia makubaliano kuhusu mzozo wa Syria. Huku mapigano yakiendelea
ndani ya Syria kwenyewe, wajumbe wamekubaliana kufanya mazungumzo zaidi.
Mazungumzo
hayo ya kimataifa yaliyozijumuisha Marekani, Urusi pamoja na mataifa
mengine saba ya kikanda yamemalizika jana Jumamosi, baada ya wajumbe
kujadiliana kwa zaidi ya saa nne, huku yakionyesha ishara kuwa yamepiga
hatua kidogo sana katika kutafuta suluhisho la kisiasa la vita vya Syria
vilivyodumu kwa miaka sita sasa.
Baada ya
miezi kadhaa ya mazungumzo, pamekuwa na matarajio kidogo ya kupatikana
kwa ufumbuzi wa haraka wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,
John Kerry na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov walipokutana na
wanadiplomasia waandamizi kutoka Saudi Arabia, Iran, Iraq, Uturuki,
Qatar, Misri na Jordan kwenye mji wa Uswisi, Lausanne, mkutano wa kwanza
kufanyika tangu kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi
uliopita. Mataifa yenye nguvu ya Ulaya hayakuhudhuria mkutano huo,
lakini yatakutana katika mkutano mwingine tofauti na Marekani, mjini
London, Uingereza leo Jumapili.
Wakati
mapigano yaliyosababisha mauaji ya watu 400,000 na mamilioni wengine
kuyakimbia makaazi yao yakiendelea, Lavrov amesema pande hizo
zimejadiliana kuhusu masuala ya kuvutia, huku Kerry akisema wanatafuta
njia nyingine mpya ya amani na kuangalia namna ya kuyafufua tena
makubaliano ya kusitisha mapigano. Kerry amesema wamekubaliana kuendelea
kwa mazungumzo ya ngazi ya juu.
Masuala
muhimu ambayo bado hayajafikiwa ni pamoja na kuyashawishi makundi mengi
yenye silaha kuheshimiwa kwa mpango wa kusitisha mapigano,
kuwatenganisha waasi wanaoungwa mkono na mataifa ya Magharibi, Ghuba na
Uturuki kutoka kwenye makundi yanayotambuliwa kama ya kigaidi, kufungua
njia ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kufika kwenye maeneo
yaliyozingirwa na kukubaliana kuhusu mpango utakaosaidia kupatikana kwa
suluhisho la kisiasa ambao jumuiya ya kimataifa na mataifa yenye nguvu
ya kikanda yana mitazamo tofauti kuhusu nafasi ya Rais wa Syria, Bashar
al-Assad na mustakabali wa nchi hiyo.
Makubaliano kuhusu mapambano na IS
Suala
pekee ambalo wajumbe hao wanaonekana kukubaliana, ni kuwarejesha nyuma
na kuwasambaratisha wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu-IS, ambao
wanaendesha mashambulizi Syria na Iraq. Kuvunjika kwa mpango wa
kusitisha mapigano uliofikiwa kati ya Marekani na Urusi, kumefatiwa na
ghasia kubwa mjini Aleppo, ambako vikosi vya Syria vikiungwa mkono na
wapiganaji wa Iran na ndege za kivita za Urusi, wanaendesha mashambulizi
kwa lengo la kuukomboa mji huo wa mashariki kutoka kwa waasi
waliofanikiwa kuuzingira na kuwafanya kiasi ya raia 250,000 kukwama.
Kukombolewa
kwa Aleppo, mji uliokuwa na wakaazi wengi nchini Syria kabla ya kuzuka
kwa vita na ambao umeharibiwa vibaya, kutakuwa ni ushindi
utakaosababisha wahanga wengi. Katika hatua hiyo, Marekani, mataifa ya
Ghuba na Uturuki zitabidi kuamua iwapo zinataka kuwasaidia zaidi waasi
wenye itikadi kali, wakiwemo wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa
Al-Qaeda
Uturuki
kwa upande mmoja imelegeza msimamo wake kuhusu mustakabali wa Assad na
kupatana na Urusi wakati ikijikita zaidi katika mapambano dhidi ya IS na
kuwazuia matarajio ya Wakurdi wa Syria, ambao walivamia kaskazini mwa
Syria mwezi Agosti.
Tangu
kuanza kwa vuguvugu la maandamano ya kupigania demokrasia kwenye nchi za
Kiarabu mwaka 2011, mzozo wa Syria umetumbukia katika pande mbalimbali
na kusababisha kuibuka kwa maeneo mengi ya mapambano, hivyo kuchangia
kuwepo makundi kadhaa ya waasi yakiwemo yale yenye wapiganaji ambao ni
raia wa Syria na wageni, mahasimu wa kikanda na mataifa yenye nguvu
duniani. DW
0 comments:
Post a Comment