Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu
akizungumza na Balozi wa Israel nchini Tanzania anayezihudumia pia nchi
Afrika Mashariki za Kenya na Uganda Mhe. Yahel Vilan (kulia) Ofisini
kwake jana jijini Dar es salaam. Pamoja na mambo mengine viongozi hao
wamejadili kuhusu uanzishwaji wa ushirikiano katika maeneo mbalimbali
yatayoinufaisha Tanzania na Israel kwenye sekta ya Afya.
Balozi wa
Israel nchini Tanzania anayezihudumia pia nchi Afrika Mashariki za
Kenya na Uganda Mhe. Yahel Vilan (kulia)akimweleza jambo Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu mara baada
ya kumtembelea Ofisini kwake jana jijini Dar es salaam.
Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu
(katikati) akifurahia jambo mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo
baina yake na Balozi wa Israel nchini Tanzania anayezihudumia pia nchi
Afrika Mashariki za Kenya na Uganda Mhe. Yahel Vilan (kulia) Ofisini
kwake jana jijini Dar es salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Mafunzo ya Wizara hiyo, Agnes Kimemo.
Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu
akiagana na Balozi wa Israel nchini Tanzania anayezihudumia pia nchi
Afrika Mashariki za Kenya na Uganda Mhe. Yahel Vilan (kulia) mara baada
ya mazungumzo Ofisini kwake jana jijini Dar es salaam.
* Wakubaliana Kuongeza Ushirikiano katika Mafunzo ya Wataalam wa Sekta ya Afya nchini
*Israel kuendelea kusaidia upasuaji wa watoto wenye ugonjwa wa Moyo kupitia Taasisi ya Save the Heart Institute
* Israel kusaidia Ujenzi wa Chumba cha Wagonjwa Mahututi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa UDOM
Na. Mwandishi –Wetu -Dar es Salaam
Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu
amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe.
Yahel Vilan ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao wamekubaliana
kuanzisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ambayo yatazinufaisha
Tanzania na Israel katika sekta ya Afya.
Balozi
huyo anayezihudumia nchi za Afrika mashariki Tanzania, Kenya na Uganda
katika mazungumzo na Waziri wa Afya wa Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu
ameyataja baadhi ya mambo ambayo Israel imekua ikishirikiana na Tanzania
kuwa ni pamoja na kudhamini matibabu ya moyo kwa Watoto kupitia Taasisi
ya Save Child Heart ya Israel na Mafunzo ya madaktari bingwa na Wauguzi
kutoka Hospitali mbalimbali nchini.
“Tumekuwa
na utaratibu wa kuleta madaktari ili waje watoe huduma kwa wagonjwa
pamoja na ujuzi kwa wataalam wa Tanzania” Ameeleza Balozi Vilam na
kuongeza kuwa Israel imekuwa ikitoa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalam
kutoka Tanzania hususani madaktari na Wauguzi.
Balozi
huyo amesema kuwa Israel imekua ikitoa mafunzo ya muda mfupi kwa
wataalam hususani madaktari na Wauguzi kutoka Tanzania na kuongeza kuwa
wanao mpango wa kusaidia uanzishwaji wa chumba cha wagonjwa mahututi
(ICU) katika eneo ambalo serikali ya Tanzania itapenda kuboresha huduma
hiyo.
Kwa
upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe Ummy Mwalimu ameishukuru Serikali na Wananchi wa Israel kwa
ushirikiano wanaouonyesha kwa Tanzania katika eneo la tiba hususani
kwenye udhamini wa matibabu ya watoto wenye ugonjwa wa moyo katika
taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kupitia madaktari bingwa wanaotoka
katika nchi mbali mbali ikiwemo Israel.
“Kupitia
ushirikiano na Israel, Serikali tumeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha
ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu, hadi sasa
kati ya wagonjwa 400 waliokuwa wanasubiri kupelekwa nje ya nchi kwa
ajili ya matibabu nusu yao wamepatiwa matibabu hapa nchini chini ya
utaratibu huo”. Ameeleza Mhe Ummy.
Mhe. Ummy
amemwomba Balozi wa Israel kuongeza fursa zaidi za mafunzo ya fani ya
Afya kwenye kada nyingi zaidi ikiwemo kada ya wataalam wa maabara,
wauguzi na madaktari.
Aidha, amemwomba Balozi wa Israel kuwezesha ujenzi wa chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa – Dodoma.
Amesema
hatua hiyo inatokana na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma ambapo
maboresho makubwa ya utoaji wa huduma za afya yanatakiwa ili kuweza
kuhudumia watu watakaohamia Dodoma.
0 comments:
Post a Comment