Leo, Novemba 30, 2024, Arusha ilikua jiji lenye hafla muhimu kwa wakulima wa Mkoa wa Arusha na maeneo mengine ya Tanzania. Ambapo mkutano mkuu wa wanahisa wa Tanganyika Farmers Association (TFA) ulifanyika katika viwanja vya Shopping Mall, ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Ndug. Gerald Mweli, alikua mgeni rasmi na alitoa ahadi ya kutatua changamoto zinazokikabili chama hicho, ili kuleta manufaa kwa wakulima.
Katika hotuba yake, Katibu Mkuu Mweli alieleza kuwa serikali inatambua mchango wa TFA katika kuunganisha wakulima na kutoa huduma muhimu kama vile ushauri wa kilimo na pembejeo. ambapo alikiri pia kwamba kuna changamoto ambazo wamezipeleka kwake kama vile riba kubwa kutoka kwa mabenki, ubora pembejeo, na ukosefu wa huduma za ugani. Aliahidi kushirikiana na TFA ili kutatua changamoto hizi na kuhakikisha wakulima wanapata fursa zaidi za kunufaika na huduma za chama hicho.
Mweli alisisitiza kwamba ushirikiano kati ya TFA na serikali ni muhimu ili kuimarisha uzalishaji wa wakulima na kuongeza tija katika kilimo. Aliwapongeza viongozi wa TFA kwa juhudi zao za kuboresha maisha ya wakulima na kuongeza uzalishaji kupitia kilimo cha kisasa.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TFA, Ndugu Waziri Barnaba, alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kutoa huduma bora kwa wanachama wake ili kukuza uchumi wao kupitia kilimo. Mkurugenzi Mtendaji wa TFA, Jastin Shirima, aliongeza kuwa chama hicho kitatumia ushirikiano na serikali kuhakikisha wanachama wanapata mbolea za ruzuku kupitia matawi ya TFA yaliyo kote nchini.
Hii ni ahadi muhimu kwa wakulima wa Tanzania, na inatoa matumaini ya mafanikio zaidi kwa sekta ya kilimo mkutano huo ulihudhuriwa na Wanachama zaidi ya 500 kutoka Maeneo mbalimbali hapa nchini
0 comments:
Post a Comment