WAZIRI Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa amesema msimamo wa Serikali umebaki vile vile kutoruhusu michango holela inayoendeshwa kwenye shule mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo ya yanayoulizwa na Wabunge kwa Waziri Mkuu.
Amesema michango inayoruhusiwa ni ile ya maendeleo ambapo pia baada ya kamati kukubaliana na wananchi wa eneo husika bado mwenye idhini ya kuanza kuchangisha ni Mkuu wa Wilaya wa eneo hilo.
“ Tunaposema michango holela tunajua ipo michango inayokubalika ndani ya jamii. Michango ya maendeleo ndio inayokubalika. Mfano Choo kimebomoka na gharama zake labda ni Sh Milioni mbili, Kamati ya Shule inakutana wanasema tunataka choo ili watoto wetu wapate huduma badala ya kusubiri kuandika barua, bajeti zipangwe mpaka TAMISEMI wanaweza kukubaliana hapa tuchangie mia tano tano, mchango unaenda kwenye choo.
Lakini michango hii pamoja na maamuzi hayo tumeidhibiti kidogo, pamoja na maamuzi yenu Kamati ya Shule na Kijiji kwa ajili ya maendeleo bado mwenyd idhini ya kuanza kuchangisha ni Mkuu wa Wilaya. Tumeiweka hiyo ili kuondoa watu kukaa kutengeneza michango isiyokubalika,”
“ Kwahiyo msimamo wa serikali ni ule ule kwamba hatuhitaji michango holela, michango holela ni ile mtu mmoja anakurupuka anasema kesho kila mmoja aje na Sh mia mbili mbili hazina maelekezo. Michango ya hivi haikubaliki na tumeagiza kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kusimamia kutokuepo kwa michango holela inayokwanza wazazi,” Amesema Mhe Waziri Mkuu.
0 comments:
Post a Comment