METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, December 9, 2023

LGTI YAISHAURI SERIKALI KUTOA KIPAUMBELE KWA WENYE ULEMAVU KWENYE UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Na Dotto Kwilasa,Dodoma 

SERIKALI imeshauriwa kuyafanyia kazi mapungufu ambayo hujitokeza kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa ikiwemo ushiriki mdogo wa wanawake na watu wenye ulemavu katika kugombea nafasi za uongozi ili kupata viongozi bora kwa maslahi ya Taifa.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Wataalamu pamoja na Wanazuoni wa Chuo cha Serikali za Mitaa(LGTI)Hombolo, wakati wa Kongamano la 15  la wanazuoni lililojikita kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa unaotazamwa kama kichocheo cha maendeleo nchini. 

Akizungumza kwenye kongamano hilo,Naibu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma,Utafiti na ushauri wa Chuo cha Serikali za mitaa,Dkt.Michael Msendekwa  amesema mada hiyo inatoa dira na muelekeo wa uchaguzi ujao wa serikali za mitaa mwaka 2024 na kuwataka vijana kuwa sehemu ya uelimishaji jamii kuhusu umuhimu wa kupiga kura. 

Dkt.Msendekwa amesema;"Leo  tumekuwa na Kongamano la 15 la  wanazuoni ambapo pamoja na kuongelea mambo mengi lakini kubwa ni  kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii nchini ,”amesema 

Pamoja na hayo ameeleza kuwa kutokana tafiti zilizofanywa na wanazuoni zinaonesha Wanawake hawashiriki katika kama kikamilifu kwenye uchaguzi hivyo ni jukumu la kila mwanajamii kuongeza chachu ya uelewa na faida ya kuchagua viongozi wanaofaa. 

“Wanawake wengi hawapendi kugombea bali wanachagua hivyo tumejadili ni jinsi gani wanawake wanaweza wakashiriki katika uchaguzi huo kwa sababu imeonekana kuwa ushiriki wao ni  mdogo ,baadhi yao hata hawaelewi kwanini wanapaswa kupiga kura,”amesema Dkt.Msendekwa. 

Akizungumzia mada hiyo ya uchaguzi inaenda mbali zaidi kwani wanazuoni wameona hiyo ndiyo nafasi pekee ya ushawishi wa kuchagua viongozi wazuri katika mamlaka za Serikali za mtaa  ambao wataleta maendeleo kiuchumi na kijamii bila kujihusisha na vitendo vya rushwa wala viashiria vya unyanyasaji wa kijinsia. 

“Tunaimani kuwa iwapo Serikali itachukua  maoni na mapendekezo yetu ambayo tumeyajadili hapa na  kuyafanyia,wananchi wataelewa maana ya uongozi bora na kila mtu atakuwa na utayari wa kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa sababu maoni na mapendekezo haya yamejikita katika utafiti,”amesema Dkt.Msendekwa. 

Ameeleza kuwa wao kama kiongozi cha Serikali za mitaa,wanataka maamuzi ya Serikali  yatokane na tafiti mbalimbali kwani tafiti hizo zinatoa majibu au taarifa ya vitugani tunatakiwa kufanya kwahiyo ni mada ambazo zimetokana na tafiti mbalimbali. 

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo hicho LGTI Mashala Lameck,amesema kuwa kongamano hilo la  wanataaluma ambalo hufanyika siku moja kabla ya mahafali kwa kila mwaka na wao wamechagua ya mada uchaguzi wa serikali za mtaa na kwamba wanaangalia mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi  na kijamii kwa watanzania. 

"Mada hii ni nzuri kwa maana inatupa muelekeo tunavyoelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa  wa Oktoba,2024 ,utupe sasa mawazo kupitia wanataaluma ambayo yataisaidia sasa Serikali katika kuboresha uchaguzi huo kwa hiyo kongamano la leo lina aksi kabisa tukio la mwakani la kupata viongozi katika ngazi za msingi za mamlaka za serikali za mitaa kwahiyo itachangia katika kushuari sisi kama watafiti wana taaluma kuishauri serikali maboresho yatakayofanyika ili uchaguzi wa serikali za mitaa uwe na tija mwakani,”ameeleza 

Mbali na hayo amefafanua kuwa;"Tulisukumwa kuja na mada hii mwaka huu kwa sababu sisi ni chuo cha serikali za mitaa na eneo letu ni kuishauri Serikali kupitia tafiti  na mafunzo, tukio la uchaguzi huo ambalo litafanyika mwakani linatuhusu sisi kama chuo,hivyo kwa nafasi yetu tumefanya maandalizi mapema kabla ya uchaguzi huo tukiamini kabisa uchagzi utafanyika kabla ya kongamano jingine la wanataaluma la hapo mwakani ,”amefafanua 

Amesema Kongamano hilo pia linasaidia kuweka sawa mifumo ya Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Serikali kupitia TAMISEMI namna itakavyoweza kuliendesha zoezi hilo kwa umakini ,uhuru na uwajibikaji. 

Naye Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Sospeter Mtwale ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kuhusu mada hiyo wao kama Serikali watakwenda kuyafanyia kazi kuyafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu na kanuni za serikali kwa kuwa wanaamini uchaguzi ni maendeleo na kusisitiza kuwa watahakikisha kwamba uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu. 

"Mengi yameelezwa na wanazuoni, wabobevu pamoja na wanafunzi wa chuo hiki hivyo nitoe wito kwa chuo chetu cha Hombolo kiendelee kufanya makongamano mengi zaidi na kuwaelimisha viongozi wa ngazi za Serikali za mitaa  kusimamia Tawala hizo ili  maendeleo yaende kwa wananchi ,”amesema Mtwale

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com