METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, November 24, 2023

RAIS, DKT. SAMIA ANATAKA UHUSIANO MZURI KATI YA TRA NA WAFANYABIASHARA - DKT.BITEKO


📌Aipongeza TRA kufikia asilimia 97.4 ya ukusanyaji mapato  mwaka 2022/2023

📌Ataka Wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa maslahi ya nchi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha kuwa wanatekeleza agizo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuendelea kutoa elimu ya mlipakodi kwa Watanzania na Wafanyabiashara ili kuleta ufanisi katika ukusanyaji kodi, kuendelea kuweka uhusiano mzuri kati ya Wafanyabiashara na TRA na kuhakikisha kuwa kila anayestahili kulipa kodi nchini, anailipa bila misukosuko.

Dkt. Biteko amesema hayo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika Sherehe ya utoaji Tuzo kwa Walipakodi Bora kwa mwaka 2022/2023 iliyofanyika tarehe 24 Novemba, 2023 jijini Dar es Salaam.

“Wafanyabiashara wanapaswa kulelewa ili walipe kodi zaidi, wanapaswa kufundishwa umuhimu wa kulipa kodi, na kazi hii ni ya kwenu Wizara ya Fedha na TRA na ninafurahi kwamba mnaifanya vizuri, sisi tunawatakia kila la heri katika kuifanya kazi hiyo ili mchango wa walipa kodi uendelee kuwa mkubwa ili tuweze kufikia malengo tunayojiwekea.” Alisema Dkt. Biteko

Alieleza kuwa, Serikali ya Awamu Sita itaendelea kufungua nchi ili kuvutia uwekezaji zaidi, kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, pamoja na kupambana na kutokomeza rushwa ikiwemo kwenye sehemu zinazohusisha Wafanyabiashara.

Dkt. Biteko aliipongeza TRA kwa kusimamia vizuri zoezi la ukusanyaji mapato nchini akitolea mfano malengo waliyowekewa mwaka 2022/23 ambayo wameyafikia kwa asilimia 97.4 kwani walikusanya shilingi Trilioni 24.11 kati ya shilingi Trilioni 24.76 walizopangiwa na kueleza kuwa hiyo si hatua ndogo hivyo TRA na Walipakodi wote wanastahili pongezi.

Aidha, Dkt. Biteko ametaka Wafanyabiashara watambue kuwa, kazi ya kujenga nchi si ya Serikali pekeyake bali ni ya watanzania wote hivyo amewataka kuendelea kulipa kodi ili zikajenge nchi kwa namna mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Barabara, Shule, Umeme, Maji, Hospitali zenye madawa na nyenzo nyingine ambazo uwepo wake unahitaji fedha.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com