Na Mathias Canal, Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) ameshiriki mkutano wa watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) na kuwasihi kuendelea kutafuta fursa mbalimbali za masomo katika nchi wanazoishi ili watanzania wengi waendelee kusoma nje ya nchi.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na Diaspora wenyewe na kufanyika Jijini Dar es salaam, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali inatambua umuhimu wao hivyo amewapa kazi ya kuendelea kutafuta fursa mbalimbali za masomo katika nchi wanazoishi.
“Kuwa na watanzania wengi ambao wamesoma nje ya nchi itawasaidia kuongeza ujuzi zaidi utakaowakuwa na manufaa nchini mwetu” Amesisitiza Waziri Mkenda
Waziri Mkenda ambaye ameshiriki mkutano huo kwa njia ya mtandao akiwa Jijini Dodoma amesema kuwa pamoja na kutafuta fursa za masomo nje ya nchi pia amewataka kuhakikisha wanashiriki kwa kila linalowezekana kuwawezesha wanaotaka kuja Tanzania kufundisha.
Ameyataja maeneo mahususi katika kufundisha hapa nchini kwa watu kutoka mataifa mbalimbali ambayo katika maeneo ya viaumbele katika utafiti na sayansi ambapo hakutakuwa na vikwazo vya aina yoyote.
Kadhalika, Prof Mkenda amesisitiza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaendelea kushirikiana na Diaspora hususani katika maeneo ya Sayansi, Teknolojia na Tiba ambapo ametumia fursa hiyo kuwapongeza kwa kuandaa mkutano huo kwa gharama zao huku wakisafiri kutoka nchi mbalimbali kushiriki mkutano huo.
Katika mkutano huo pia Waziri Mkenda amewaeleza washiriki hao kuwa Wizara yake imekamilisha Mapitio ya Sera na Mitalaa ambapo kwa sasa hatua ambazo zimefikiwa ni hatua za ndani za serikali kabla ya kufanyika mkutano wa wadau wote wa sekta ya elimu utakaorushwa mubashara na vyombo vya habari.
Prof Mkenda amesema kuwa mageuzi hayo ya elimu ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt SAMIA SULUHU HASSAN aliyoyatoa wakati akihutubia bunge la Tanzania tarehe 22 Aprili 2022 Jijini Dodoma.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment