METDO Tanzania

METDO Tanzania
Showing posts with label Kitaifa. Show all posts
Showing posts with label Kitaifa. Show all posts

Sunday, August 16, 2026

ULEGA: BARABARA YA KIBAONI–SITALIKE KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI KATAVI NA MAENEO JIRANI

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuwa ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike (km 70) ni muhimu katika kuchochea shughuli za kiuchumi na kufungua fursa za biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, pamoja na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na nchi jirani.

Ulega ameyasema hayo mkoani Katavi wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike, ambapo amesema Serikali itaendelea kuhakikisha inatenga na kutoa fedha kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo kukamilika kwa mujibu wa viwango na muda uliokusudiwa.

“Niwahakikishieni wananchi kuwa Mkandarasi anayejenga Barabara ya Kibaoni–Sitalike tutamlipa hivi karibuni ili aendelee na kazi. Serikali itaendelea kuhakikisha fedha zinapatikana ili mradi huu ukamilike,” amesema Ulega.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kuongeza fursa za biashara na kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko, hivyo kuchochea maendeleo ya wananchi wa Katavi na mikoa jirani.

Aidha, Ulega amesema Serikali tayari imelipa Shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Mpanda–Kigoma, huku akimtaka Mkandarasi kuhakikisha anamalizia kwa haraka ujenzi wa Daraja la Mnyamasi ili kurahisisha matumizi ya barabara hiyo na kuzuia changamoto za mawasiliano wakati wa msimu wa mvua.

“Tunataka Daraja la Mnyamasi likamilike kwa haraka ili wananchi na watumiaji wengine wa barabara wasipate usumbufu wakati wa msimu wa mvua. Wasimamizi wa mradi wanapaswa kusimama imara na kuhakikisha kazi zinafanyika kwa kasi na ufanisi,” amesema Ulega.

Waziri huyo amesisitiza kuwa wasimamizi wa miradi wanapaswa kuhakikisha maeneo yote yanayokatisha mawasiliano wakati wa mvua yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu, huku akielekeza kazi zifanyike kwa kasi bila kuathiri ubora wa miundombinu inayojengwa.

Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi, Eng. Martin Mwakabende, amesema utekelezaji wa ujenzi wa kipande cha kwanza cha barabara hiyo umegawanywa katika sehemu tatu, huku gharama ya ujenzi ikiwa ni Shilingi bilioni 88.72.

Eng. Mwakabende amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara, akisema uwekezaji huo una mchango mkubwa katika kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa Mkoa wa Katavi na mikoa jirani.

Ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuimarisha mtandao wa barabara nchini, kurahisisha usafirishaji na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi katika maeneo yanayounganishwa na barabara hiyo.










Share:

Tuesday, January 6, 2026

VYUO VIKUU VYAZINDUA MRADI WA KIMKAKATI KUKABILI MSONGO WA MAWAZO KWA VIJANA

 

Na Mathias Canal, Dodoma‎

‎Katika hatua inayotajwa kuwa mwanga mpya kwa vijana wanaokabiliwa na changamoto za afya ya akili, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimezindua rasmi mradi wa u’GOOD TevuAfya, unaolenga kushughulikia kwa vitendo matatizo ya afya ya akili kwa vijana, hususan wanaoishi mijini na pembezoni mwa miji.

‎

‎Uzinduzi wa mradi huo umefanyika Januari 6, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Afrika Mashariki, ukihusisha viongozi wa chuo, watafiti, wadau wa maendeleo pamoja na wanafunzi.

‎

‎Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Lughano Kusiluka, amesema mradi wa u’GOOD TevuAfya ni miongoni mwa miradi 23 ya kimataifa inayotekelezwa chini ya programu ya Good Life, huku miradi minane ikitekelezwa Tanzania.

‎

‎“Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa Tanzania inaendelea kujijengea heshima na nafasi muhimu katika ramani ya utafiti wa kisayansi duniani,” amesema Profesa Kusiluka.

‎

‎Ameeleza kuwa ushindani wa kupata ufadhili wa miradi ya utafiti ni mkali, hivyo mafanikio ya watafiti wa Tanzania kupata miradi hiyo yanaonesha ubora wa kazi na umuhimu wa tafiti zinazolenga kutatua matatizo halisi ya jamii.

‎

‎Kwa mujibu wa Profesa Kusiluka, changamoto za afya ya akili kwa vijana zimeongezeka kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo hali ngumu za kiuchumi, mabadiliko ya mifumo ya kifamilia, msongo wa mawazo, matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii pamoja na kasi ya maendeleo ya teknolojia za kidijitali.

‎

‎“Afya ya akili si tatizo la vijana pekee, ni suala la jamii nzima. Familia, wazazi na mazingira yanayowazunguka vijana vina mchango mkubwa,” amesema, akisisitiza umuhimu wa tafiti shirikishi zitakazosaidia kupata suluhisho endelevu.

‎

‎Aidha, ametoa wito wa kuimarishwa kwa elimu ya uraia kwa vijana ili kuwajengea uzalendo, kujiamini na kuiona Tanzania kama nchi ya fursa na matumaini, akibainisha kuwa misingi ya maadili na utambulisho wa kitaifa ina mchango mkubwa katika ustawi wa afya ya akili.

‎Kwa upande wa wanafunzi, Akley Omary wa UDOM amesema afya ya akili ni uwezo wa mtu kukabiliana na mawazo chanya na hasi yanayotokana na changamoto za maisha na mazingira ya kijamii.

‎Amesema wanafunzi wengi hukumbwa na msongo wa mawazo unaotokana na changamoto za kifedha, matatizo ya kifamilia na mazingira magumu ya masomo, huku kukosa mahitaji muhimu kama chakula, vifaa vya masomo na fedha za matumizi vikizidi kuathiri ustawi wao wa kisaikolojia.

‎Naye David Julius, mwanafunzi wa Shahada ya Business Information System, amesema dhana potofu kwamba afya ya akili ni sawa na wazimu imekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana kutafuta msaada.

‎“Afya ya akili ni uwezo wa mtu kufanya maamuzi sahihi na kuchanganua mambo kwa ufanisi, kufeli masomo na kushindwa kufanya maamuzi sahihi mara nyingi hutokana na msongo wa mawazo,” amesema.

‎Kwa upande wake, Rebeca Omari Kabanda, mwanafunzi wa Information Security Engineering, amesema ukosefu wa ajira ni moja ya changamoto kubwa zinazowaathiri vijana kisaikolojia, hasa pale matarajio ya maisha baada ya kuhitimu yanapogonga mwamba.

‎Ameongeza kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA na mitandao ya kijamii yanaweza kuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu na msaada wa kisaikolojia kwa vijana, akisisitiza umuhimu wa kujiepusha na tabia hatarishi na mahusiano yasiyo rasmi yanayoweza kuathiri afya ya akili na maendeleo ya kielimu.

‎Mradi wa u’GOOD TevuAfya unatarajiwa kutoa mapendekezo ya kisera pamoja na mbinu za vitendo zitakazosaidia kuboresha afya ya akili kwa vijana na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kujenga taifa lenye vijana wenye afya njema ya mwili na akili.

Share:

Wednesday, December 31, 2025

DKT. NATU APONGEZA UBUNIFU NA UBORA WA JARIDA LA HAZINA YETU

 

Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amepongeza ubunifu na ubora wa Jarida la Hazina Yetu Toleo la Tano ambalo limeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Fedha.

Ametoa pongezi hizo wakati akipokea Jarida hilo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mwamba alisema Jarida hilo ambalo limeendela kuwa bora na kufika kila mahali duniani kwa njia ya kidigitali ni nyenzo muhimu katika kuwasilisha taarifa sahihi, za wazi na kwa lugha inayoeleweka kuhusu shughuli, mafanikio na mipango ya Wizara ya Fedha.

Dkt. Mwamba alipongeza jitihada za Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa kuendelea kuboresha mawasiliano na uelimishaji kwa umma pamoja na ubunifu na weledi unaooneshwa katika uandaaji wa Jarida hilo, akibainisha kuwa limeendelea kuwa chombo muhimu cha kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya fedha na uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Bw. Benny Mwaipaja alisema kuwa Jarida la Hazina Yetu linalenga kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha pamoja na mchango wake katika maendeleo ya Taifa, akiahidi kuendelea kuliboresha ili liwe chombo chenye tija zaidi katika mawasiliano ya serikali.

Jarida la “Hazina Yetu Toleo la Tano” limesheheni maarifa mbalimbali kupitia Makala bora kabisa, habari, matukio ya picha na matangazo mbalimbali na linapatikana kwa njia ya nakala ngumu (hard copies) na nakala tete (soft copies) kupitia mitandao ya kijamii ya Wizara na wadau wengine wa habari pamoja na Tovuti ya Wizara ya Fedha www.mof.go.tz 


Share:

Sunday, December 7, 2025

BMH YASOGEZA HUDUMA ZA AFYA KARIBU NA WANANCHI, YAHAMASISHA UCHANGIAJI DAMU, MSALATO MNADANI - KATIKA KUADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA.

 

Na Meleka Kulwa- Dodoma 

Desemba 6, 2025 Jijini Dodoma 

‎

‎Hospitali ya Benjamin Mkapa imepeleka huduma za afya katika Viwanja vya Mnadani Msalato jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto yanayoadhimishwa kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka, kwa lengo la kuwafikia wananchi wasiopata kwa urahisi huduma za afya.

‎

‎Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Bw. Teophory Mbilinyi, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amewahimiza wananchi wa Msalato na Watanzania wenye changamoto za kiafya kufika hospitalini  kwa matibabu ya kina ya huduma za kibingwa, akisisitiza kuwa kwa pamoja watajenga taifa.

‎

‎

‎Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Wauguzi, Bi. Mwanaidi Makao; aliwasisitiza wananchi kufika katika banda hilo ili kujipatia huduma mbalimbali zinazopatikana hapo, na aliahidi timu ya BMH itarudi katika awamu zingine katika kutoa elimu na huduma katika eneo hilo.

‎

‎Pia kabla ya hapo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Ubunifu na Mratibu wa Huduma za Masuala ya Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto, Bi. Hindu Ibrahim, amesema kuwa timu ya madaktari, na wataalamu wengine imefika Msalato Mnadani kutoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi, hawakufika kwa ajili ya kutoa elimu pekee bali pia kutoa huduma za vitendo ikiwemo upimaji wa afya, uchangiaji damu na huduma za afya ya akili.

‎

‎Bi. Hindu amesema kuwa Msalato Mnadani ni eneo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu wanaofika kwa shughuli mwisho wa wiki; baadhi hukosa muda wa kufika hospitalini. Kusogeza huduma katika eneo hilo kumewezesha kuwafikia wananchi ambao hawajapima afya kwa muda mrefu.

‎

‎

‎Baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo, akiwemo Ratifa Abdalah mkazi wa Miyuji, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili uokoa maisha ya watanzania Wenye matatizo na uhitaji wa damu. Aidha, amesema kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa inatoa huduma bora.

‎

‎Kwa upande wake, Bi.Sauda Omary mkazi wa Msalato amesema kuwa  wananchi wanapaswa kupima afya na kujua hali zao. Akibainisha kuwa huduma zilizofikishwa Msalato ni msaada mkubwa kwa kuwa zimewasogezea huduma wananchi waliokuwa wakipata ugumu wa kufika hospitalini. aidha, Aliishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuendelea kusogeza huduma karibu na jamii.










‎

Share:
Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com