METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, January 6, 2023

Rais Samia Aleta Mapinduzi ya Mawasiliano Nchini-Mhe Kundo

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Kundo Andrea Mathew (MB) kulia akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Mafia Mheshimiwa Mhandisi Martini S. Tnemo mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili kufanya ziara yake yenye lengo la Kukangua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi leo Januari 4, 2023
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Kundo Andrea Mathew (MB) aliesimama akielezea jambo kwa viongozi wa wilaya ya Mafia juu ya ziara yake yenye lengo la Kukangua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi leo Januari 4, 2023


Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuleta mapinduzi katika sekta ya mawasiliano nchini kwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya sekta hiyo kwa lengo la kutatua changamoto ya mawasiliano sambamba na kuvutia uwekezaji. 


Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew alipowasili wilayani Mafia mkoani Pwani kwa ajili ya kufanya ziara yake yenye lengo la kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa redio TBC Taifa na uhakiki wa anwani za makazi.


“Najivunia kazi kubwa ya kimapinduzi ndani ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliyofanya na Mheshimiwa Rais kwa vile wakati naingia katika wizara hii ambayo inabeba miundombinu yote ya kimawasiliano nchini bajeti yake haikuwa inaakisi uhalisia wa kazi kubwa ambayo inatakiwa kufanyika, bajeti ya wizara hii ilikuwa shilingi bilioni nane kwa mwaka lakini Mheshimiwa Rais alivyoingia madarakani kwa awamu yake ya kwanza alipitisha bajeti ya shilingi bilioni 230,” ameeleza Mhe. Naibu Waziri Kundo.


Amesisitiza: “Shilingi bilioni 230 maana yake ni miradi mingi zaidi ya ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano, ajira za moja kwa moja, na miundombinu inapoimarika zaidi huduma za mawasiliano zinazidi kupatikana kwa urahisi na gharama zake zitaendelea kuwa nafuu.”

Aidha, Mheshimiwa Naibu Waziri Kundo ametolea mfano faida za uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta hiyo kuwa mwaka 2020 gharama za kupiga simu kutoka mtandao mmoja hadi mwingine kwa dakika ilifika wastani wa shilingi 60 lakini kwa sasa kupiga simu ni wastani wa shilingi 30 kwa mitandao yote.


Sambamba na hayo, Mheshimiwa Naibu Waziri kundo, amebainisha baadhi ya jitihada zilizofanywa na Serikali kuwa ni uwekezaji wa miundombinu ambapo hadi sasa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeunganishwa na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ili uweze kutoa huduma pamoja na maeneo mengine ya mpakani. 


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mheshimiwa Mhandisi Martin Ntemo, ameeleza kuwa kufuatia jitihada hizo za Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano, wilaya hiyo ina minara 10 inayotoa huduma za mawasiliano ya simu kwa mitandao ya Airtel, TTCL, Vodacom, Tigo, Zantel na Halotel.

“Huduma ya mawasiliano kwa sasa imefikia asilimia 69.9, wananchi hutumia huduma hizi kwa ajili ya kurahisisha masuala ya kijamii ambayo ni kupashana taarifa mbalimbali, elimu kwa mtandao, sanaa na michezo pamoja na shughuli za kiuchumi," ameeleza Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Ntemo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com