METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, January 7, 2023

ELIMU BILA ADA HAIMAANISHI MCHANGO WA HIYARI USITOLEWE-WAZIRI MKENDA

Na Mathias Canal, Rombo

Serikali imeondoa ada elimu ya msingi hadi kidato cha sita ili kuongeza uwezekano wa watanzania wengi kuoata elimu kwa ufasaha mkubwa.

Imesema kuwa kufuatia kuondoa ada haimaanishi wadau wa maendeleo wasichangia kwa hiari yao ambapo pia serikali inaendelea kuwaomba wadau hapo kuendelea kuchangia kwenye shule walizosoma.

Mbunge wa Jimbo la Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 7 Januari 2023 wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kutembelea shule ya sekondari Bustani iliyopo kata ya Mrao Keryo Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro akiwa katika ziara ya kikazi.

Amewapongeza wadau wa maendeleo hususani katika sekta ya elimu ambao wameendelea kujitolea kwa ajili ya maendeleo katika sekta ya elimu.

Prof Mkenda pia amewapongeza wadau hao kwa kujitolea kwao katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo vyoo, ujenzi wa madarasa, ujenzi wa mabweni na maktaba.

"Kazi ya ujenzi wa miundombinu ni jukumu la serikali lakini wananchi wanaoendelea kujitolea kuchangia wanaunga mkono juhudi za serikali kwa vitendo" Amekaririwa Waziri Mkenda

Prof Mkenda amewataka wananchi wa Rombo kuungana kwa pamoja na kuwa na ushirikiano kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwani siasa sio porojo bali siasa ni maendeleo.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com