Na Mathias Canal, WEST-Kilimanjaro
Serikali imejipanga kuanza ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) kote nchini ambapo kiasi cha Bilioni 100 kimetengwa kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.
Ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi VETA unatarajiwa kuanza hivi karibuni katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo jambo litakaloimarisha elimu ujuzi kwa wanafunzi kote nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 8 Januati 2023 wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kisangiro Kata ya Mwanga akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mkenda amesema kuwa ujenzi huo wa VETA katika wilaya zote nchini ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ambaye ameelekeza wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuimarisha elimu ujuzi.
"Changamoto yetu kubwa ilikuwa ni kupata ardhi, hatuna hela ya kulipa fidia hivyo tuliomba Halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya kuanza ujenzi na karibu Halmashauri zote zimeitikia wito huo, tunasisitiza tu umuhimu wa kuhakikisha hati zinakabidhiwa haraka iwezekanavyo" Amekaririwa Mhe Mkenda
Waziri Mkenda ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Mwanga kupitia Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Abdallah Mwaipaya pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe Joseph Tadayo kwa kuonyesha mfano kwa vitendo upatikanaji wa eneo pamoja na hati kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Prof Mkenda amewataka wakurugenzi wa Halmashauri kote nchini kujitathmini kwani kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kutozwa michango mingi kwa lazima kwa wanafunzi jambo ambalo ni hatari na sio afya kwenye sekta ya elimu nchini.
Waziri Mkenda amesema kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kuchangia kwa hiari maendeleo katika ujenzi wa miundombinu ya shule na sekta ya elimu kwa ujumla wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kaskazini Bi Monica Mbele amesema kuwa kazi kubwa iliyopo kwa sasa ni utekelezaji wa kuanza ujenzi kwani taratibu zote za kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa VETA Wilayani Mwanga umekamilika sambamba na upatikanaji wa hati.
Pia amewasihi wanafunzi katika wilaya ya Mwanga kujiunga na chuo cha VETA kwa ajili ya mafunzo pindi itakapokamilika.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment