METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, January 29, 2023

NAIBU WAZIRI MASANJA AWATAKA WANANCHI KUPANDA MITI NA KUTUNZA MAZINGIRA

 







NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mary Masanja amewahimiza wananchi kuwa wahifadhi wa mazingira kwa kupanda miti ili kuepukana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoikumba dunia kama ukame, mafuriko n.k.

Naibu Waziri Masanja amesema hayo katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 46 ya Chama cha Mapinduzi yanayotarajia kufikia kilele chake Februari 5, 2023

“Nataka niwakumbushe kwamba uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu hivyo tuyatunze mazingira ili yaweze kututunza” amesisitiza Mhe. Masanja.

Ameongeza kuwa Ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kila mwananchi ahakikishe anapanda mti na kuutunza ili uweze kukua.

Amesema kufuatia maelekezo Rais, Wizara ya Maliasili na Utalii  itahamasisha  wananchi kupanda miti hususan katika kipindi hiki cha mvua kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kijani.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja ametembelea Shule ya Sekondari Muhandu iliyopo katika Halmashauri ya jiji la Mwanza kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi na wananchi wa eneo hilo kuwa na utamaduni wa kupanda miti.

 “CCM ndicho chama kinachoongoza nchi hivyo tukiunge mkono ili kuwaletea wananchi maendeleo  kwa hiyo pia tumuunge mkono Mheshimiwa Rais ili tuweze kufikisha maendeleo ya wananchi pale mlipo” amesema  Marry Masanja.

Maadhimisho ya Miaka 46 ya Chama cha Mapinduzi yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda ambaye alikuwa mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti UWT Taifa, Zainab Shomari pamoja na viongozi wengine wa UWT Taifa na wanachama wa jumuiya hiyo kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com