Na Mwandishi Wetu, MUFINDI
SHIRIKA la PELUM Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi Mkoani Iringa kupitia linatarajia kutoa hati miliki za kimila 795 kwa
wananchi wa Vijiji vya Ugesa, Isaula,
Magunguli na Usokami na Mukungu waliopimiwa ardhi zao kupitia Mpango wa
Matumizi bora ya ardhi.
Hayo yamesemwa jana (juzi) Wilayani Mufindi na
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Leonard Jaka wakati wa zoezi la upitishaji wa mpango wa
matumizi bora ya ardhi uliofanywa katika kijiji hicho na Shirika la PELUM
Tanzania kupitia mradi wa Ushiriki wa wananchi katika Sekta ya Kilimo (CEGO).
Jaka alisema Wananchi wa kijiji cha Makungu pamoja
na vijiji jirani katika Halmashauri hiyo kuchangamkia fursa hiyo ya kupima
ardhi zao ili kuweza kuepekana na migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiathiri
shughuli za maendeleo ya wananchi Wilayani humo.
Jaka alisema mpango huo ni muhimu kwa kuwa unatoa
kipaumbele kwa wajane, wagane, walemavu, wazee na watu wenye kipato cha chini
kupata hati miliki ya ardhi na hivyo aliwataka wananchi ambao hawajapimiwa
ardhi zao wahakikishe wanajipanga ili waweze kufikiwa na mpango huo.
“Kupimwa kwa ardhi zenu kutasaidia kuepukana na
migogoro ya ardhi, kujihakikishia ulinzi wa ardhi,kuwa na umiliki halali wa
kisheria wa ardhi, kuongezeka kwa thamani ya ardhi pamoja na kurahisisha upatakanaji
wa mikopo kwa kuweka ardhi yako kama dhamana,” alisema Jaka.
Aidha Jaka
aliwakumbusha wananchi wa kijiji cha Makungu wajibu wao katika kusimamia
kikamilifu mpango kwa kutoingilia au kuuuza maeneo ya huduma za kijamii ambayo
yaliyopimwa na kuutaka Uongozi wa Serikali ya Kijiji kuchukua hatua za kisheria
kwa wote watakaobainika kwenda kinyume na sheria ndogo walizojiwekea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Makungu, Donatus
Mnoga alisema kijiji chake pamoja na vijiji jirani wamekuwa katika hali ya
sintofahamu ya kugombea mipaka toka mwaka 2008 bila ufumbuzi jambo lililokuwa
lilileta mkanganyiko wa idadi halisi ya vitongoji vilivyopo katika mamlaka yake.
Alisema kupitia mradi wa CEGO unaotekelezwa kwa
ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, hivi sasa Viongozi wa Serikali
za Vijiji hivyo wameweza kukutanishwa na hatimaye kupata suluhu ya kudumu ya
tatizo ikiwemo kurejeshwa kwa kitongoji cha Lole katika kijiji cha Makungu
hatua inayokifanya kijiji hicho kuwa vitongoji vitatu kwa sasa.
Naye Mkazi wa Kijiji hicho cha Mukungu, Gaudensio
Mwagala alilishukuru Shirika la PELUM Tanzania na Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi kwa kuweka utaratibu wa kuwapimia ardhi yake na kusema jambo litalosaidia
kuondoa utata wa urithi wa umiliki wa ardhi yake katika siku za usoni.
Mradi wa Ushiriki wa wananchi katika Sekta ya
Kilimo (CEGO) unaofadhiliwa na Shirika la Misaada La Marekani (USAID)
unatekelezwa katika Halmashauri sita zilizopo katika Mikoa ya Dodoma, Morogoro
na Iringa.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment