METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, January 31, 2022

MADIWANI WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILEMELA MWANZA WAPITISHA MPANGO WA BAJETI WA BIL. 77.194 KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023




Maganga Gwensaga – Mwanza

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza, limepitisha  mpango wa bajeti wa Shilingi bilioni 77.194 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023  pamoja na mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi  kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Bajeti hiyo ambayo kuandaliwa  kwake kumezingatia mambo mbalimbali ukiwemo mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano 2021/2022-2025/2026, Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025, Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs)2020-2025, Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 pamoja na maoni ya wadau mbalimbali ulipitishwa Januari 28 Mwaka 2022.

Akisoma taarifa ya mpango huo kabla ya kupitishwa na Madiwani wa halmashauri hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary alitaja kuongezeka kwa mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani kutoka  10,172,706,000.00 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia 13,524,000,000.00 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 32.9.

Alisema ongezeko hilo linatokana na Halmashauri kuanza kutumia na kutekeleza sheria ndogo mpya zilizoboreshwa zinazoipa Halmashauri uwezo wa kukusanya mapato kwa nguvu za kisheria sambamba na kuchukua hatua Zaidi za kisheria kwa wanaoshindwa kulipa ada na tozo mbalimbali.

“ Sababu nyingine ni kuendelea kuimarika kwa takwimu mbalimbali za vyanzo vya mapato, uwepo wa ongezeko la ukusanyaji, wananchi kuongeza ari ya ulipaji kodi inayotokana na elimu wanavyopewa, usimamizi wa mikataba ya ukusanyaji mapato na uundwaji wa timu maalumu ya ufuatiliaji mapato pamoja na kuajiri vibarua kwa ajili ya kuongeza nguvu za ufuatiliaji.” Alisema Mhandisi Modest

Aidha aliyataja baadhi ya mafaniko yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ikiwemo kuendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati ya ujenzi wa Stendi ya Mabasi na maegesho ya Malori katika eneo la Nyamhongolo ambapo kazi ya ujenzi imefikia 90%

“ Mafaniko mengine ni ukamilishwaji wa ujenzi wa vyumba 15 vya madarasa, ujenzi wa matundu 36 ya vyoo, utengenezaji wa madawati 375 katika shule za Msingi, ujenzi wa vyumba 128 katika shule 24 za Sekondari, ununuzi wa madawa katika vituo vyote vya afya pamoja na ununuzi wa Jenereta katika kituo cha afya cha Buzuruga.” Alisema Mkurugenzi

Aliyataja baadhi ya mafaniko yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2021 Halmashauri iliweza kuongeza vyumba vya madarasa 97, viti na meza 4850, ofisi 28 katika shule za Sekondari 26, ujenzi wa vyumba 6 vya maabara, ujenzi wa matundu 48 ya vyoo pamoja na usimamizi mkamilifu wa ujenzi wa mindombinu na utengenezaji wa madawati katika shule za msingi yenye thamani ya shilingi 372,031,259.70.

“ Mheshimiwa Mwenyekiti naomba sasa baraza lako liweze kupokea na kupitisha mpango wa bajeti ya halmashauri ya manispaa ya  ilemela kwa mwaka wa fedha 2022-2023 wenye jumla ya fedha bilioni 77.194 kati ya fedha hizo bilioni 19.123 kwa ajili ya ruzuku ya miradi ya maendeleo, Bilioni 42.819 mishahara, Biilioni 1.727.568 ruzuku ya matumizi ya kawaida, bilioni 13.524  kwa ajili ya mapato ya ndani naomba kuwasilisha.” Alimaliza Mhandisi Apolinary

Baada ya Mkurugenzi kusoma taarifa hiyo Madiwani waliweza kuijadili na hatimaye kuipitisha  huku baadhi yao wakiwapongeza wataalamu wa Halmshauri hiyo wakisema kwamba bajeti hiyo imeendaliwa kitaalamu na itakuwa mkombozi wa wana Ilemela.

Walisema wana furaha kulingana na bajeti ilivyokuwa imekuwa bajeti ya mfano na wanamatumaini itaenda kuwagusa wananchi moja kwa moja hasa kutokana na kiasi cha fedha kilichotengwa katika eneo la afya, elimu, ardhi na hasa mpango wa ulipaji fidia kwa wakati kwa wananchi ambao watachukuliwa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com