Maganga Gwensaga – Mwanza
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya manispaa ya
Ilemela Mkoani Mwanza, limepitisha mpango wa bajeti wa Shilingi bilioni 77.194 kwa
kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023
pamoja na mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Bajeti hiyo ambayo kuandaliwa kwake kumezingatia mambo mbalimbali ukiwemo
mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano 2021/2022-2025/2026, Dira ya Taifa
ya maendeleo ya mwaka 2025, Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs)2020-2025,
Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 pamoja na maoni ya
wadau mbalimbali ulipitishwa Januari 28 Mwaka 2022.
Akisoma taarifa ya mpango huo kabla ya kupitishwa na
Madiwani wa halmashauri hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi
Modest Apolinary alitaja kuongezeka kwa mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani
kutoka 10,172,706,000.00 kwa mwaka wa
fedha 2021/2022 hadi kufikia 13,524,000,000.00 kwa mwaka wa fedha 2022/2023
sawa na ongezeko la asilimia 32.9.
Alisema ongezeko hilo linatokana na Halmashauri kuanza
kutumia na kutekeleza sheria ndogo mpya zilizoboreshwa zinazoipa Halmashauri uwezo
wa kukusanya mapato kwa nguvu za kisheria sambamba na kuchukua hatua Zaidi za
kisheria kwa wanaoshindwa kulipa ada na tozo mbalimbali.
“ Sababu nyingine ni kuendelea kuimarika kwa takwimu
mbalimbali za vyanzo vya mapato, uwepo wa ongezeko la ukusanyaji, wananchi
kuongeza ari ya ulipaji kodi inayotokana na elimu wanavyopewa, usimamizi wa
mikataba ya ukusanyaji mapato na uundwaji wa timu maalumu ya ufuatiliaji mapato
pamoja na kuajiri vibarua kwa ajili ya kuongeza nguvu za ufuatiliaji.” Alisema
Mhandisi Modest
Aidha aliyataja baadhi ya mafaniko yaliyopatikana
kutokana na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ikiwemo kuendelea
na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati ya ujenzi wa Stendi ya Mabasi na
maegesho ya Malori katika eneo la Nyamhongolo ambapo kazi ya ujenzi imefikia
90%
“ Mafaniko mengine ni ukamilishwaji wa ujenzi wa
vyumba 15 vya madarasa, ujenzi wa matundu 36 ya vyoo, utengenezaji wa madawati
375 katika shule za Msingi, ujenzi wa vyumba 128 katika shule 24 za Sekondari,
ununuzi wa madawa katika vituo vyote vya afya pamoja na ununuzi wa Jenereta
katika kituo cha afya cha Buzuruga.” Alisema Mkurugenzi
Aliyataja baadhi ya mafaniko yaliyopatikana kutokana
na utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa kipindi cha
kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2021 Halmashauri iliweza kuongeza vyumba vya
madarasa 97, viti na meza 4850, ofisi 28 katika shule za Sekondari 26, ujenzi
wa vyumba 6 vya maabara, ujenzi wa matundu 48 ya vyoo pamoja na usimamizi
mkamilifu wa ujenzi wa mindombinu na utengenezaji wa madawati katika shule za
msingi yenye thamani ya shilingi 372,031,259.70.
“ Mheshimiwa Mwenyekiti naomba sasa baraza lako
liweze kupokea na kupitisha mpango wa bajeti ya halmashauri ya manispaa ya ilemela kwa mwaka wa fedha 2022-2023 wenye
jumla ya fedha bilioni 77.194 kati ya fedha hizo bilioni 19.123 kwa ajili ya
ruzuku ya miradi ya maendeleo, Bilioni 42.819 mishahara, Biilioni 1.727.568
ruzuku ya matumizi ya kawaida, bilioni 13.524
kwa ajili ya mapato ya ndani naomba kuwasilisha.” Alimaliza Mhandisi
Apolinary
Baada ya Mkurugenzi kusoma taarifa hiyo Madiwani
waliweza kuijadili na hatimaye kuipitisha huku baadhi yao wakiwapongeza wataalamu wa
Halmshauri hiyo wakisema kwamba bajeti hiyo imeendaliwa kitaalamu na itakuwa
mkombozi wa wana Ilemela.
Walisema wana furaha kulingana na bajeti ilivyokuwa
imekuwa bajeti ya mfano na wanamatumaini itaenda kuwagusa wananchi moja kwa
moja hasa kutokana na kiasi cha fedha kilichotengwa katika eneo la afya, elimu,
ardhi na hasa mpango wa ulipaji fidia kwa wakati kwa wananchi ambao
watachukuliwa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
No comments:
Post a Comment